

Lugha Nyingine
Rais wa Uturuki Erdogan akutana na mwanadiplomasia mwandamizi wa China Wang Yi juu ya uhusiano wa pande mbili
![]() |
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kulia) akipeana mkono na Wang Yi, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, wakati wakikutana mjini Ankara, Uturuki, Julai 26, 2023. (Ikulu ya Uturuki/Xinhua) |
ANKARA - Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amekutana na mwanadiplomasia mwandamizi wa China Wang Yi kujadili juu ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.
Erdogan amemwomba Wang, ambaye ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kuwasilisha salamu zake za dhati kwa Rais Xi Jinping wa China na kuongeza kuwa Uturuki na China zote ni nchi zenye ushawishi wa kimataifa na umuhimu wa ushirikiano wao unavuka mipaka ya nchi hizo mbili.
Erdogan amesisitiza Uturuki inashikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja na kusema nchi yake haioni maendeleo ya China kuwa tishio.
"Uturuki iko tayari kuongeza mabadilishano ya ngazi ya juu na China kupitia mifumo kama vile Kamati ya Ushirikiano kati ya Serikali na Kamati ya Pamoja ya Uchumi na Biashara," amesema Erdogan, na kuongeza kuwa nchi yake iko tayari kuimarisha kuunganisha kwa Pendekezo la Uturuki la Ukanda wa Kati na Pendekezo la China la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), ili kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika biashara, nishati, utalii na nyanja nyinginezo, na kuinua uhusiano kati ya Uturuki na China kufikia kiwango kipya.
Rais Erdogan pia amesisitiza kuwa nchi yake haiungi mkono NATO kuongeza shughuli zake katika eneo la Asia-Pasifiki na iko tayari kufanya mawasiliano na uratibu na China katika masuala ya kimataifa na kikanda, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Ukraine.
Kwa upande wake Wang, amewasilisha salamu za Rais wa China kwa Rais Erdogan. Amemwambia kwamba China inampongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa rais na inaiunga mkono Uturuki katika kudumisha uhuru na kufuata njia ya maendeleo inayoendana na hali yake ya kitaifa.
Wang ameeleza nia ya China ya kutumia vyema utaratibu wa Kamati ya Ushirikiano kati ya Serikali ya China na Uturuki ili kuendeleza kwa pande zote ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali, kuwezesha ujenzi wa BRI, kufikia kiwango cha juu cha ushirikiano wa kunufaishana, na kutoa mchango chanya katika ufufukaji wa uchumi wa Dunia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma