Benki ya maendeleo ya China yaongeza msaada kwa ajili ya miradi ya kuhifadhi maji

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 31, 2023

Benki ya Maendeleo ya China imeongeza msaada wa kifedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya kuhifadhi maji nchini China katika nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Benki hiyo imesema katika kipindi hicho ilitoa mikopo yenye thamani ya yuan bilioni 110.2 (sawa na dola bilioni 14.45 za Kimarekani), ili kuimarisha ujenzi wa miradi ya uhifadhi wa maji. Hadi sasa benki hiyo imetoa msaada wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mikubwa ya uchepushaji wa maji, usambazaji wa maji na umwagiliaji, ili kuboresha usambazaji wa maji na kuhakikisha usalama wa maji nchini China.

Kutokana na China kuwa katika kipindi muhimu cha kupambana na mafuriko, Benki ya Maendeleo ya China imetoa mikopo hiyo ili kusaidia kuimarisha kingo za mabwawa ya kuhifadhi maji, kukarabati mabwawa yaliyochakaa, na kuimarisha msaada wa kifedha ili kukabiliana na majanga yanayotokana na maji.

Benki hiyo pia ilitoa mikopo inayolenga kufadhili usafishaji wa maji, urejeshaji wa kiikolojia wa mito mikuu, na kuhakikisha upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha