

Lugha Nyingine
China yaongeza kasi ya kuwapanga upya wakazi wa eneo la Beijing-Tianjin-Hebei baada ya maafa yaliyosababishwa na mvua
Ili kukabiliana na dhoruba kali iliyosababisha mvua na mafuriko ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa mjini Beijing na mikoa ya jirani, mamlaka zinahamasisha juhudi za kila namna kuwalinda watu dhidi ya athari zilizosababishwa na mvua hiyo. Katika siku chache zilizopita mji wa Beijing umeshuhudia mvua kubwa kunyesha tangu ulipoanza kuweka rekodi miaka 140 iliyopita.
Waokoaji wakimhamisha mwanakijiji aliyejeruhiwa katika kijiji cha Shuiyuzi kilichoathiriwa vibaya na mafuriko katika eneo la Mentougou, mjini Beijing. Agosti 1, 2023. (Xinhua /Ju Huanzong)
Maeneo ya Mentougou na Fangshan kusini na magharibi mwa mji wa Beijing ni maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko. Zaidi ya polisi 2,000 wa mji wa Beijing wametumwa katika eneo la Fangshan kusaidia shughuli za uokoaji na kutoa misaada.
Katika mji wa Tianjin, mamlaka za huko zimewahamisha watu 66,000 na kuchukua hatua za kukabiliana na mafuriko kutoka mitoni.
Watu wakiwa kwenye mashua ya uokoaji kuelekea kwenye kituo cha kusafirishwa katika eneo salama la Fangshan Beijing, Agosti 2, 2023. (Xinhua/Ren Chao)
Mji wa Zhuozhou ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi katika mkoa wa Hebei. Mamlaka za eneo hilo zimeanzisha vikundi 28 vya uokoaji vikiwa na watu 8,755 ili kusaidia kazi ya uokoaji. Watu hao wameshirikiana na askari wa huko na timu nyingine za wataalamu wa uokoaji.
Wanajeshi wanagawa chakula na maji kwa abiria wa treni namba K396 katika Mji wa Miaofengshan wa eneo la Mentougou, mjini Beijing. Agosti 2, 2023. (Xinhua/Ju Huanzong)
Serikali ya China imetenga Yuan milioni 100 kusaidia kazi za ukarabati baada ya maafa kwa ajili ya mji Beijing na mkoa wa Hebei. Fedha kutoka kwenye bajeti kuu zitatumika kusaidia ujenzi wa miundombinu na huduma za umma katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mvua na mafuriko.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma