China yaimarisha kazi za ukarabati katika maeneo ya kaskazini yaliyoathiriwa na mafuriko

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 08, 2023

Waokoaji wakiwa kwenye kazi ya kuondoa maji katikati ya mji wa Zhuozhou, Mkoani Hebei China, Agosti 7, 2023. (Xinhua/Mu Yu)

Waokoaji wakiwa kwenye kazi ya kuondoa maji katikati ya mji wa Zhuozhou, Mkoani Hebei China, Agosti 7, 2023. (Xinhua/Mu Yu)

SHIJIAZHUANG/BEIJING, Agosti 7 (Xinhua)

Wakati maji ya mafuriko yanapungua katika Mkoa wa Hebei na mji wa Beijing kaskazini mwa China, juhudi za kutoa misaada katika maeneo hayo zimebadilika kutoka uokoaji wa dharura, na kuwa kurejesha hali ya kawaida kwa maisha ya watu haraka iwezekanavyo.

Katika mji wa Zhuozhou, moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi mkoani Hebei, wakazi waliohamishwa hapo awali wameanza kurejea nyumbani. Wakazi, wafanyakazi wa kujitolea na waokoaji wanashiriki kikamilifu kwenye kazi za uchimbaji, kuua vijidudu, na kuondoa maji ili kurekebisha sehemu zilizoharibiwa kutokana na mafuriko. Shirika la Umeme la Zhouzhou limesema hadi kufikia Jumatatu asubuhi, umeme umerejeshwa katika jumuiya 93 za makazi huko Zhuozhou, huku zaidi ya asilimia 90 ya vitongoji vya maeneo ya karibu na mijini vikirejeshewa huduma hiyo.

Idara ya usafiri wa umma ya Mkoa wa Hebei imesema sehemu 1,470 za barabara katika mkoa wa Hebei ambazo awali zilikatika kutokana na mafuriko zilikuwa zimefunguliwa hadi kufikia saa 6 mchana wa Jumapili. Hali hii imewezekana kutokana na uwekaji wa madaraja ya dharura na kufunguliwa kwa barabara za muda, kuhakikisha usafiri wa wafanyakazi wa misaada na vifaa.

Idara hiyo pia imeimarisha ukaguzi katika sehemu za barabara ambazo hazifikiki kwa urahisi, na kuondoa uchafu mara moja kwenye miteremko, kushughulikia maporomoko ya udongo kwenye barabara, na kupunguza hatari zinazoweza kutokea.

Idara ya kilimo na mambo ya vijiji ya Mkoa wa Hebei imesema ili kupunguza hasara kwenye shughuli za kilimo, mkoa huo unafanya uchunguzi wa kina na tathmini ya kiwango cha uharibifu wa mazao, mifugo na ufugaji wa samaki katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.

Ofisa anayesimamia shamba la familia katika Wilaya ya Anping ya Hebei, Bw. Zhao Xiaoming, amesema wasiwasi wake sasa umepungua baada ya kuona kiwango cha maji mashambani kinapungua kwa kiasi kikubwa. Amesema serikali imewapatia vifaa vya kusukuma maji, ambavyo vimesaidia kuokoa mazao yao kwa mwaka huu.

Zaidi ya pampu 460 za maji zimesambazwa katika mashamba yaliyoathirika huko Anping kwa ajili ya kusaidia kusukuma maji kwenye mifereji. Timu ya wataalamu imetoa mwongozo kwenye tovuti kwa ajili ya kudhibiti magonjwa na wadudu, na kuhusu upandaji upya wa mazao.

Katika mji wa Handan, timu ya kuzuia magonjwa ya wanyama imefanya kazi ya kukusanya kuku waliokufa kutoka kwenye mashamba ya ufugaji wa kuku, huku mizoga ikisafirishwa kwa uangalifu hadi kwenye kituo maalum ambapo inatupwa kwa usalama.

Katika mji wa Beijing, serikali ya eneo la Mentougou imesema jumla ya kilomita 440 za barabara za mashambani katika sehemu tisa ambazo zilikumbwa na mvua kubwa mapema wiki iliyopita, zilikuwa zimefunguliwa tena kuanzia saa nne usiku wa Jumapili.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha