

Lugha Nyingine
Siku ya kumi ya Michezo ya Vyuo Vikuu ya Dunia ya Chengdu: China yaweka rekodi mpya siku moja kabla ya michezo kufungwa
Huang Zigan wa China akiwa katika fainali ya kupiga mbizi kutoka kwenye jukwaa la mita 10 kwa wanaume kwenye michezo ya vyuo vikuu ya dunia inayoendelea huko Chengdu, Agosti 7, 2023. (Xinhua/Wu Gang)
Ikiwa imebaki siku moja kabla ya michezo ya vyuo vikuu ya dunia inayoendelea huko Chengdu kufungwa, China imeweka rekodi ya kupata medali 103 za dhahabu.
Baada ya mashindano mengi kukamilika katika siku ya 10 ya michezo ya vyuo vikuu ya dunia inayoendelea huko Chengdu, China iliweka rekodi kwa kujikusanyia medali 178, zikiwemo 103 za dhahabu.
Wapiga mbizi wa China walipata medali nne zaidi za dhahabu kwa upande wa wanaume, kwenye timu mchanganyiko, timu ya wanaume na timu ya wanawake, huku wakikusanya medali zote 15 za dhahabu kwenye mchezo huo, pamoja na fedha tano na shaba moja. Korea Kusini ilimaliza katika nafasi ya pili kwa kupata medali nne za fedha na nne za shaba.
Waogeleaji wa China pia walijipatia medali nne zaidi za dhahabu katika siku ya mwisho ya mechi ya mchezo wa kuogelea na kuweka rekodi mbili za michezo ya vyuo vikuu ya dunia FISU kwenye mita 50 mtindo huru kwa wanawake, na mita 4x100 kwa wanaume kupokezana.
Baada ya kupata medali zote za dhahabu katika michezo saba ya awali huko Chengdu, bingwa wa Olimpiki Zhang Yufei aliongeza medali mbili zaidi kwenye mkusanyiko wake wa medali kwenye mita 50 mtindo huru kwa wanawake na mita 4x100 kupokezana kwa wanawake.
Zhang Yufei wa China akisherehekea ushindi wa mchezo wa kuogelea mita 50 kwa mtindo huru kwenye michezo ya vyuo vikuu ya dunia inayoendelea huko Chengdu, Agosti 7, 2023. (Xinhua/Wu Gang)
Li Bingjie pia alipata ushindi wa medali ya dhahabu wakati wa kukamilisha matukio yote manane, na kuhitimisha safari kwenye michezo ya vyuo vikuu ya dunia kwa ushindi mnono kwenye mchezo wa kuogelea mita 400 kwa wanawake.
Katika bwawa hilo hilo, China iliifunga Italia mabao 12-7 na kushinda fainali ya mchezo wa polo kwenye maji kwa upande wa wanawake, huku timu ya wanaume ya China ikishika nafasi ya saba baada ya ushindi wa mabao 9-7 dhidi ya Japan.
Siku ya mwisho ya mashindano ya mchezo wa mpira wa vinyoya ilikuwa ni mashindano kati ya waasia pekee, na fainali tatu kati ya tano zikiamuliwa kati ya wachezaji wenza. Taipei ya China ilitawala kwenye mchezo mchanganyiko, huku China ikifanya vizuri kwenye upande wa wanaume na wanawake. Mataji hayo ya wachezaji wa pekee pia yalikwenda kwa wachina baada ya Wang Zhengxing na Han Yue kuwashinda wapinzani wao kutoka Thailand na Korea Kusini katika fainali za wanaume na wanawake.
Li Yongzhen wa China (katikati) akisherehekea siku yake ya kuzaliwa baada ya mechi ya kugombea medali ya shaba ya mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume dhidi ya Iran kwenye michezo ya vyuo vikuu ya dunia inayoendelea huko Chengdu, Agosti 7, 2023. (Xinhua/Xu Bingjie)
Li Yongzhen ambaye alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa alichangia pointi 13 wakati China ilipoishinda Iran kwa seti mfululizo na kutwaa medali ya shaba kwenye mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume. Mabingwa watetezi Italia waliishinda Poland kwa seti 3-0 na kujinyakulia medali ya dhahabu.
Kwenye fainali ya mchezo wa foil kwa wanaume, bingwa wa mchezo wa mmoja mmoja Cheung Ka-long aliiongoza Hong Kong, China na kushinda pointi 45-33 dhidi ya Ufaransa, huku China ikilazimika kusalia katika nafasi ya nne. Baada ya kupata medali ya dhahabu kwa upande wa wanawake, Ufaransa inaongoza kwa kutwaa medali tisa zikiwemo tatu za dhahabu. China imeshika nafasi ya pili kwa kuwa na dhahabu tatu, fedha moja na shaba mbili.
Mechi za kuwania medali ya dhahabu na shaba kwa wanaume zitakuwa mechi pekee siku ya Jumanne, huku sherehe ya ufungaji ikifanyika jioni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma