

Lugha Nyingine
Mwezi Julai, Mwaka 2023 ndiyo mwezi wenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa tangu Mwaka 1880
Watoto wakicheza ili kupoza joto la mwili katika bustani ya chemchemi iliyoko katikati mwa Jiji la Houston, Texas, Marekani, Juni 15, 2023. (Picha na Chen Chen/Xinhua)
LOS ANGELES - Mwezi Julai, Mwaka 2023 ulikuwa mwezi wenye joto kali zaidi kuliko mwezi mwingine wowote katika rekodi ya joto duniani tangu Mwaka 1880, kwa mujibu wa uchambuzi uliotolewa na Taasisi ya Goddard ya Masomo ya Anga ya Juu (GISS) ya Shirika la Taifa la Anga ya Juu la Marekani (NASA) siku ya Jumatatu.
Mwezi Julai, Mwaka 2023 ulikuwa na joto la nyuzi 0.43 Fahrenheit (nyuzi 0.24 Selsiasi) kuliko Julai nyingine yoyote katika rekodi ya NASA, na ulikuwa na joto la nyuzi joto 2.1 Fahrenheit (nyuzi 1.18 Selsiasi) kuliko wastani wa hali joto ya mwezi Julai kati ya Mwaka 1951 na 1980, kwa mujibu wa uchambuzi huo.
"Takwimu za NASA zinathibitisha kile ambacho mabilioni ya watu kote duniani walihisi: halijoto ya mwezi Julai 2023 ilifanya mwezi huo kuwa wenye joto zaidi katika rekodi. Katika kila kona ya nchi, Wamarekani hivi sasa wanajionea athari za tabianchi," Msimamizi wa NASA Bill Nelson amesema.
Watu wakipoza joto la mwili karibu na chemchemi huko Washington, D.C., Marekani, Julai 11, 2023. (Picha na Aaron Schwartz/Xinhua)
Maeneo ya Amerika Kusini, Afrika Kaskazini, Amerika Kaskazini na Rasi ya Bahari ya Antaktika yalikuwa ya joto sana, na halijoto iliongezeka karibu nyuzi joto 7.2 Fahrenheit (nyuzi 4 Selsiasi) juu ya wastani, kwa mujibu wa data hizo za NASA.
Joto la juu la uso wa bahari lilichangia rekodi ya joto ya mwezi Julai, kwa mujibu wa NASA. Uchambuzi wa shirikika hilo unaonyesha halijoto ya bahari katika eneo la kitropiki la mashariki la Bahari ya Pasifiki, ikiwa ni ushahidi wa El Niño ambayo ilianza kujitokeza mnamo Mei 2023.
Kwa ujumla, joto kali la msimu huu wa joto limeweka makumi ya mamilioni ya watu chini ya tahadhari za joto na limehusishwa na magonjwa na vifo vya mamia ya watu vinavyotokana na joto, kwa mujibu wa NASA.
Data hizo za NASA zinaonesha, Miezi mitano ya Julai yenye joto kali zaidi tangu Mwaka 1880 yote imetokea katika miaka mitano iliyopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma