

Lugha Nyingine
Kumbukumbu za mapambano ya miaka mingi yaliyofanywa na watu wa China na Korea Kusini dhidi ya uvamizi wa Japan
Han See-jun, Mkuu wa Jumba la Uhuru la Korea, akizungumza kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua huko Cheonan, Korea Kusini, Juni 12, 2023. (Xinhua/Zhou Siyu)
BEIJING/SEOUL - Mnamo Agosti 15, 1945, tukio la kihistoria lilijitokeza wakati Japan ilipotangaza rasmi kujisalimisha bila masharti katika Vita vya Pili vya Dunia (WWII). Siku hii muhimu inaadhimishwa kama Siku ya Taifa ya Ukombozi nchini Korea Kusini, kuashiria kukombolewa kwa Peninsula ya Korea kutoka kwa miongo kadhaa ya ukoloni dhalimu wa Japan.
Kuanzia Mwaka 1910 hadi 1945, Peninsula ya Korea ilikuwa chini ya ukoloni wa Japan ya Kibeberu. Katika kipindi hiki, watu wa peninsula hiyo walipitia ukandamizaji na ugandamizaji, lakini pia walionyesha uhimilivu wa ajabu katika mapambano yao dhidi ya uvamizi wa Japan.
Wakati huo, wapigania uhuru wengi katika peninsula hiyo ya Korea walikuja China baada ya kupoteza nchi yao kwa Japan. Walipigana bega kwa bega na jeshi la China dhidi ya wavamizi wa Japan hadi kupatikana kwa ushindi wa vita dhidi ya ufashisti.
Urafiki wa pande zote kati ya watu wa China na Korea Kusini, ulioanzishwa wakati wa mapambano hayo ya pamoja, umedumu tangu wakati huo.
Kwa miaka mingi, mawasiliano na ushirikiano kati ya Jumba la Makumbusho ya Vita vya Watu wa China vya Kupambana na Uvamizi wa Japan mjini Beijing na Jumba la Uhuru wa Korea huko Cheonan, yamekuwa yakistawi.
Mapambano ya pamoja
Wanamapinduzi wa China walitoa msaada mkubwa kwa wapigania uhuru wa Korea, amesema Han See-jun, Mkuu wa Jumba la Uhuru la Korea, katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua.
Miongoni mwa kumbi saba za maonyesho katika jumba hilo, mbili zinaonyesha mapambano dhidi ya uvamizi wa Japan yaliyofanywa na wapigania uhuru kutoka kwenye peninsula katika China Bara. Katika kumbi hizi pia zimeoneshwa data kuhusu mashirika ya China na watu wa China waliounga mkono na kupigana pamoja na wapigania uhuru wa Korea.
"Historia ya kupigana bega kwa bega dhidi ya ufashisti inashuhudia urafiki wa pande zote kati ya China na Korea Kusini," amesema Luo Cunkang, msimamizi wa Jumba la Makumbusho la Vita vya Watu wa China vya Kupambana na Uvamizi wa Japan, akielezea matumaini ya kuhifadhi historia katika kumbukumbu ya watu wa nchi zote mbili.
Ushirikiano wa karibu
Majumba mawili ya makumbusho ya China na Korea Kusini yakiwa yalianzishwa Mwaka 1987, yanawasilisha historia ya kupinga uvamizi wa Japan ya nchi zao, katika kujibu vitabu vya kiada vya historia ya Japan Mwaka 1982 ambavyo vilipotosha historia yake ya ukoloni na kuremba uvamizi wake.
Han amesisitiza kuwa, China, Korea Kusini na nchi nyingine za Asia, ambazo zimekuwa wahanga wa uvamizi wa Japan, zinapaswa kuungana kujifunza na kukumbuka uzoefu wa kihistoria wa mapambano ya pamoja dhidi ya Japan, na kuitaka Japan kuomba radhi na kutafakari makosa yake ya kivita.
Picha hii iliyopigwa Juni 12, 2023 ikionyesha mwonekano wa nje wa Jumba la Uhuru la Korea lililoko Cheonan, Korea Kusini. (Xinhua/Zhou Siyu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma