

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China akutana na Waziri wa Biashara wa Marekani, akitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano
Waziri Mkuu wa China Li Qiang akikutana na Waziri wa Biashara wa Marekani Gina Raimondo ambaye yuko ziarani nchini China kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing Agosti 29, 2023. (Xinhua/Rao Aimin)
BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana mjini Beijing na Waziri wa Biashara wa Marekani Gina Raimondo ambaye yuko ziarani nchini China, akitoa wito kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana.
Kwenye mazungumzo yao yaliyofanyika Jumanne, Waziri Mkuu Li amesema uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani ni wa kunufaishana na kiasili ni wenye faida kwa pande zote. Amesema, kuingiza siasa katika masuala ya kiuchumi na kibiashara na kuvumisha dhana ya usalama si tu kwamba kutaathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wa pande mbili na hali yakuaminiana, bali pia kutadhoofisha maslahi ya kampuni na watu wa nchi hizo mbili, na kutakuwa na athari mbaya kwa uchumi wa Dunia.
Waziri Mkuu Li amedhihirisha kuwa China ni nchi kubwa zaidi inayoendelea na Marekani ni nchi kubwa iliyoendelea, pande hizo mbili zinapaswa kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana, kupunguza mivutano na mapambano, na kuhimiza kwa pamoja kuimarisha uchumi wa Dunia na kukabiliana na changamoto za kimataifa.
Amesema, uhusiano mzuri na thabiti kati ya China na Marekani unazinufaisha nchi hizo mbili na Dunia, na China inafurahi kuona kwamba Marekani hivi karibuni imesisitiza mara kwa mara kuwa imejitolea kurejea kwenye ajenda iliyowekwa na marais wa nchi hizo mbili huko Bali.
"Kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kufanya ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote ni njia sahihi kwa China na Marekani kuendana pamoja. Tunatumai kuwa upande wa Marekani utashirikiana na China katika kuchukua hatua zaidi za kivitendo na zenye manufaa ili kudumisha na kuendeleza uhusiano wa pande hizo mbili." ameongeza.
Amesema, China inafanya juhudi za kufungua mlango wake kwenye kiwango cha juu na kufanya juhudi za kuweka mazingira ya biashara ya kiwango cha kimataifa, yenye mwelekeo wa soko yanayotawaliwa na mfumo mzuri wa kisheria.
Kwa upande wake Raimondo amesema, serikali ya Rais Biden inaunga mkono maendeleo ya uchumi wa China na uboreshaji wake wa maisha ya watu, haina nia ya kuzuia maendeleo ya China, haitaki kutengana kiuchumi na China, iko tayari kudumisha mawasiliano na uhusiano wa kawaida wa kiuchumi na kibiashara, na iko tayari kuhimiza maendeleo thabiti ya uhusiano wa pande mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma