Mkutano wa Viongozi wa Kundi la 20 wahitimishwa kwa ahadi ya kuharakisha kufikia ukuaji wa uchumi wenye nguvu, endelevu, uwiano na jumuishi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 11, 2023

Mkutano wa 18 wa viongozi wa Kundi la 20 (G20) umehitimishwa Jumapili ya Septemba 10 huko New Delhi, India. Mkutano huo umepitisha Azimio la Viongozi wa Mkutano wa G20 wa New Delhi na kuahidi kuchukua hatua madhubuti ili kukabiliana na changamoto duniani.

Azimio hilo linasema, mambo yanayozuia ukuaji na utulivu wa uchumi wa dunia bado yapo, na changamoto na hatari zisizoisha zimerudisha nyuma mchakato wa kutekeleza Ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030. Azimio linasisitiza muundo wa maendeleo unaounga mkono mageuzi ya dunia ambayo ni endelevu, jumuishi na ya haki, na kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayeachwa nyuma.

Azimio hilo linasisitiza tena kwamba changamoto zinapaswa kukabiliwa kupitia kustawisha tena ushirikiano wa pande nyingi, mageuzi na ushirikiano wa kimataifa. Kuhakikisha kwamba nchi zinazoendelea zina uwakilishi na sauti kubwa zaidi katika mchakato wa kufanya maamuzi wa mashirika ya uchumi na fedha ya kimataifa.

Azimio linatoa wito kwa nchi zilizoendelea kutekeleza ahadi zao rasmi za msaada wa maendeleo, linaeleza kuunga mkono Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo Endelevu wa Mwaka 2023, na kusisitiza utekelezaji wa “Mfumokazi wa Bioanuwai wa Kimataifa wa Kunming-Montreal.”

Azimio hilo linakaribisha Umoja wa Afrika kuwa mwanachama wa kudumu wa Kundi la 20, na litaendelea kuunga mkono Afrika kupitia Mpango wa G20 (Mkutano wa Hangzhou) wa Kuunga Mkono Maendeleo ya Viwanda ya Nchi za Afrika na Nchi zenye Maendeleo Duni.

Mkutano ujao wa viongozi wa Kundi la 20 utafanyika mwezi wa Novemba, 2024 huko Rio de Janeiro, Brazil.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha