Uwekezaji wa China katika uhifadhi wa maji wafikia rekodi ya juu katika kipindi cha kati ya Januari na Agosti mwaka huu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 14, 2023
Uwekezaji wa China katika uhifadhi wa maji wafikia rekodi ya juu katika kipindi cha kati ya Januari na Agosti mwaka huu
Picha hii ya angani iliyopigwa Agosti 10, 2023 ikionyesha mandhari ya mji wa kale wa Taierzhuang kando ya Mfereji Mkuu wa Beijing-Hangzhou katika Wilaya ya Taierzhuang iliyoko Mji wa Zaozhuang, Mkoa wa Shandong, Mashariki mwa China. (Xinhua/Guo Xulei)

BEIJING - China imewekeza kiasi kinachovunja rekodi cha Yuan bilioni 985.6 (kama dola bilioni 137.09 za Kimarekani) kwenye ujenzi wa vifaa vya kuhifadhi maji katika kipindi cha miezi minane ya kwanza ya mwaka huu, amesema Waziri wa Rasilimali za Maji wa China, Li Guoying kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jumatano.

Amesema, jumla ya miradi 23,600 ya kuhifadhi maji imezinduliwa katika kipindi hiki, ambayo pia ni ya juu katika historia.

Ujenzi wa miradi ya kuhifadhi maji umetoa ajira zaidi ya milioni 1.97 kuanzia Januari hadi Agosti, na kutoa "uungaji mkono mkubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi," Li amesema.

Mbali na kuendeleza ujenzi wa miradi ya kuhifadhi maji, China pia imezidisha juhudi zake za kulinda na kurejesha mifumo ya ikolojia ya maji safi.

Amesema, maji yenye mita za ujazo takriban bilioni 7 yaliingizwa kwenye mito na maziwa 48 katika Bonde la Mto Haihe Mwaka 2022 na mito mingi Kaskazini mwa China imekuwa na maji yanayotiririka na ya safi, wakati mito mingi zaidi imerejea kuwa na uhai tena.

China imetekeleza mifumo ya "chifu wa mto" na "chifu wa ziwa", ambapo viongozi wa serikali za mitaa wanapewa jukumu la kulinda mifumo ya maji ndani ya maeneo wanayasimamia. Mpaka sasa,machifu wa mito na maziwa zaidi ya milioni 1.2 wameteuliwa.

Satelaiti za kuhisi kwa mbali, droni na teknolojia nyingine pia zimetumika sana kuimarisha ukaguzi, usimamizi na ulinzi wa kila siku wa mito na maziwa.

“Kupitia utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kubana matumizi ya maji, China imepata maendeleo thabiti katika kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji na kuongeza ufahamu wa watu juu ya umuhimu wa kuokoa matumizi ya maji,” Li amesema.

Mwaka 2022, matumizi ya maji ya China kwa kila Yuan 10,000 ya Pato la Taifa yalipungua kwa asilimia 33 kutoka kiwango cha Mwaka 2015, na matumizi yake ya maji kwa kila yuan 10,000 ya ongezeko la thamani ya viwandani yalipungua kwa asilimia 50.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha