

Lugha Nyingine
Spika wa Bunge la Canada ajiuzulu kwa kualika bungeni mwanajeshi mstaafu wa itikadi za Nazi
Picha rasmi isiyo na tarehe ikimwonyesha msemaji wa Bunge la Canada, Anthony Rota, akitabasamu mbele ya kamera. (Kwa hisani ya North Bay News)
OTTAWA - Spika wa Bunge la Canada, Anthony Rota, amejiuzulu wadhifa wake siku ya Jumanne huku kukiwa na utata juu ya mwaliko wake kwa mwanajeshi mstaafu aliyepigia upande wa kikosi cha kijeshi cha Itikadi za Nazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Rota ametangaza uamuzi wake huo wa kujiuzulu baada ya kukutana na viongozi wa Bunge kutoka pande zote kwenye Kilima cha Bunge Jumanne alasiri.
"Bunge hili liko juu yetu sote. Kwa hivyo, lazima nijiuzulu kama spika wenu," Rota amewaambia wabunge wakati akitangaza kujiuzulu kabla ya kipindi cha maswali bungeni siku ya Jumanne.
Katika hotuba yake, Rota pia amesisitiza tena majuto yake kwa kosa la kumtambua mtu huyo katika Bunge. Rota amesema kuwa "utambuzi wa umma" alioutoa kwa askari wa zamani wa Itikadi za Nazi "umesababisha maumivu kwa watu binafsi na jamii," ikiwa ni pamoja na Wayahudi, Wapolandi na "manusura wengine wa ukatili wa Nazi."
Tangazo la kujiuzulu kwa Rota lilipokelewa kwa shangwe katika ukumbi wa bunge.
Kujiuzulu kwa Rota kunakuja huku kukiwa na ufichuzi kwamba wabunge wa Bunge la Canada walitoa pongezi za kusimama na kupiga makofi mengi kwa Yaroslav Hunka, raia wa Ukraine mwenye umri wa miaka 98, muda mfupi baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kulihutubia Baraza la Wawakilishi (the House of Commons) ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini Canada. Siku ya Jumamosi, ilikuja kujulikana kuwa Hunka alikuwa sehemu ya kitengo cha Jeshi la Nazi kilichopigania uhuru wa Ukraine wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Wabunge wa Canada, wakiwemo wale wa chama cha Kiliberali cha Rota, walikuwa wakitoa shinikizo kumtaka aondoke kwenye kiti cha spika kwa misingi ya maadili.
Rota, ambaye alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Chama cha Kiliberali Mwaka 2004, amekuwa spika wa Baraza la Wawakilishi tangu Mwaka 2019.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma