

Lugha Nyingine
Mjadala Mkuu wa UN wahitimishwa kwa kutoa wito wa kujitolea kupambana na changamoto za Dunia, kujenga mshikamano
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kwenye jukwaa na kwenye skrini) akizungumza katika ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 19, 2023. (Xinhua/ Li Rui)
UMOJA WA MATAIFA - Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) umehitimishwa Jumanne, huku viongozi wa Dunia wakisema kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa jukwaa kuu la kutoa suluhu za changamoto za binadamu.
Katika hotuba yake ya kuhitimisha, Rais wa Baraza Kuu Dennis Francis amesisitiza kujitolea kusikoyumba kwa Umoja wa Mataifa kuleta amani, ustawi na uendelevu duniani.
"Umoja wa Mataifa unaendelea kuzingatia changamoto za pamoja za wakati wetu," amesema.
Takwimu za awali zinaonyesha kuwa mkutano huo wa mwaka huu uliofanyika kwa wiki nzima umeshuhudia umuhimu mkubwa zaidi wa viongozi wa kimataifa waliokutana ana kwa ana huko New York tangu kuanza kwa janga la UVIKO-19.
Mkutano huo umehusisha viongozi wakuu wa nchi 88, wakuu wa serikali 42 na mawaziri zaidi ya 650. Maafisa wakuu hao walichukua fursa ya ushiriki huu mkubwa na kufanya mikutano ya pande mbili zaidi ya 2,000.
Mjadala Mkuu ulifunguliwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Septemba 19, ukilenga kurejesha imani na mshikamano wa kimataifa katika nyakati za sasa za changamoto.
Katika wiki iliyopita, wakuu wa nchi na serikali waliangazia changamoto mbalimbali, kuanzia tishio la dharura za mabadiliko ya tabianchi hadi wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya teknolojia za akili bandia.
Pia wamesisitiza jukumu kuu la Umoja wa Mataifa na haja ya kufanya mageuzi ya shirika hilo ili kufaa kwa madhumuni haya.
Mwaka huu, mada ya mjadala mkuu ni: "Kujenga upya imani na kuamsha mshikamano wa kimataifa: Kuharakisha hatua za Ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu kuelekea amani, ustawi, maendeleo na uendelevu kwa wote."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma