Tanzania yaitambua China kama soko jipya la kimkakati la utalii

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 07, 2023

Wanafunzi kutoka Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakicheza ngoma ya simba kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Utalii ya Kiswahili jijini Dar es Salaam

Wanafunzi kutoka Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakicheza ngoma ya simba kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Utalii ya Kiswahili jijini Dar es Salaam, Tanzania, Oktoba 6, 2023. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)

DAR ES SALAAM – Serikali ya Tanzania imetangaza siku ya Ijumaa kwamba imezitambua nchi za China, Russia na India kama masoko mapya ya kimkakati ya utalii ya nchi hiyo.

“Wakati ambapo Tanzania inaelekea katika kukuza sekta yake ya utalii, tumegundua masoko kadhaa ya kimkakati ya utalii yakiwemo China, Russia na India,” amesema Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania, Thereza Mugobi.

Mugobi ameyasema hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Utalii ya Kiswahili katika mji wa bandari wa Dar es Salaam, ambayo yamevutia washiriki zaidi ya 150 na wanunuzi zaidi ya 100 wa kimataifa kutoka nchi zaidi ya 20 duniani.

Amesema, pamoja na masoko mapya ya utalii ya kimkakati yaliyoainishwa, Tanzania ina uwezo wa kufikia lengo lake la kuvutia watalii milioni 5 wa kimataifa ifikapo Mwaka 2025.

Akifungua maonyesho hayo ya utalii kwa niaba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Angellah Kairuki amesema serikali inachukua hatua zinazolenga kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania katika ramani ya kimataifa.

Ameongeza kuwa sekta ya utalii nchini Tanzania inachangia asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni na asilimia 17.5 ya pato la taifa.

Hafla ya ufunguzi wa maonyesho hayo ya utalii yatakayofanyika kwa siku tatu, yenye kaulimbiu isemayo "Utalii Unaowajibika kwa Ukuaji Jumuishi," ilijumuisha maonyesho ya kitamaduni ya wanafunzi kutoka Taasisi ya Confucius ya China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na washiriki kutoka India, Indonesia, Rwanda, Msumbiji na nchi mwenyeji, Tanzania.

Wasanii wakicheza ngoma ya kijadi kutoka Rwanda kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Utalii ya Kiswahili jijini Dar es Salaam, Tanzania, Oktoba 6, 2023. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)

Wasanii wakicheza ngoma ya kijadi kutoka Rwanda kwenye hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Utalii ya Kiswahili jijini Dar es Salaam, Tanzania, Oktoba 6, 2023. (Picha na Emmanuel Herman/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha