

Lugha Nyingine
Reli ya kisasa iliyojengwa na China nchini Kenya yasifiwa kwa manufaa yake mengi
Ujumbe wa mabalozi wanaowakilisha mashirika na nchi zao nchini Kenya ukitembelea kituo cha kuruhusu treni kuondoka katika Stesheni ya Nairobi ya Reli ya Mombasa-Nairobi mjini Nairobi, Kenya, Oktoba 6, 2023. (Xinhua/Wang Guansen)
NAIROBI - Reli ya kisasa ya Mombasa-Nairobi (SGR) iliyojengwa na China imekuwa kichocheo kwa mageuzi nchini Kenya tangu ilipozinduliwa miaka sita iliyopita, mabalozi wanaowakilisha mashirika na nchi zao nchini Kenya wamesema.
Wakizungumza wakati wa safari ndani ya treni ya abiria ya SGR kutoka Nairobi, Kenya, hadi mji wa pwani wa Mombasa siku ya Ijumaa, wajumbe hao wameeleza kuwa mradi huo wa reli ya kisasa umeleta manufaa mengi ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa watu na mizigo, kustawisha biashara na uwekezaji kando ya ukanda wake wenye urefu wa kilomita 472.
Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian alijumuika na mabalozi hao kutoka Russia, Iran, Saudi Arabia, Brazil, Afrika Kusini, Misri, Hungary, na Ethiopia katika safari iliyo salama, yenye ufanisi na ya haraka iliyohakikishwa na treni ya abiria ya SGR.
Ujumbe wa mabalozi hao pamoja Maimunah Mohd Sharif, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Umoja wa Mataifa la Makazi ya Binadamu (UN-HABITAT), walitazama video za uenezi za kuadhimisha mwaka wa sita tangu kuzinduliwa kwa reli hiyo ya SGR ya Mombasa-Nairobi Mei 31, 2017, na kutembelea kituo cha kuruhusu treni, na mnara wa China na Kenya kabla ya kuanza safari.
Balozi wa Russia nchini Kenya Dmitry Maksimychev amesema safari hiyo imempa fursa ya kuona manufaa ya ushirikiano kati ya China na Kenya, akiongeza kuwa mradi huo wa SGR ni kielelezo cha uhamishaji wa teknolojia ili kuchochea maendeleo jumuishi.
Aidha, Maksimychev ameeleza kuwa mradi huo ulitilia maanani maadili ya ulinzi wa ikolojia wakati wa ujenzi wake, na pia kuimarisha muunganisho kati ya miji mikubwa miwili ya Kenya ambayo ni vituo vya biashara na uchukuzi.
Ikiwa ni matunda ya awali ya Pendekezo la China la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), reli ya SGR ya Mombasa-Nairobi pia ni mradi kitangulizi wa mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa Dira ya 2030 ya Kenya.
Ni sehemu muhimu ya Ukanda wa Kaskazini wa Mtandao wa Reli wa Afrika Mashariki na ilichaguliwa na jarida la kila wiki la Engineering News-Record kuwa Mradi Bora wa Reli wa Kimataifa wa Mwaka 2018.
Watoto wakisubiri kupanda treni kwenye Stesheni ya Nairobi ya Reli ya Mombasa-Nairobi mjini Nairobi, Kenya, Oktoba 6, 2023. (Xinhua/Wang Guansen)
Ujumbe wa mabalozi wanaowakilisha mashirika na nchi zao nchini Kenya ukitazama burudani katika Stesheni ya Nairobi ya Reli ya Mombasa-Nairobi mjini Nairobi, Kenya, Oktoba 6, 2023. (Xinhua/Wang Guansen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma