Nchi 15 zachaguliwa kuwa wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 11, 2023

Maofisa wa mkutano wakisubiri kura za mwisho za nchi wajumbe  wakati wa uchaguzi wa nchi wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 10, 2023. (Loey Felipe/Picha Ya UN/ Xinhua)

Maofisa wa mkutano wakisubiri kura za mwisho za nchi wajumbe wakati wa uchaguzi wa nchi wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 10, 2023. (Loey Felipe/Picha Ya UN/ Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA - Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limechagua nchi 15 kuwa nchi wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lenye nchi wajumbe 47 kwa awamu ya miaka mitatu kuanzia Januari 1, 2024.

Kupitia kura ya siri siku ya Jumanne, Burundi, Cote d'Ivoire, Ghana, Malawi (kwa Afrika); China, Indonesia, Japan, Kuwait (kwa Asia-Pasifiki); Albania, Bulgaria (kwa Ulaya Mashariki); Brazili, Cuba, Jamhuri ya Dominika (kwa Amerika ya Kusini na Karibiani); Ufaransa, Uholanzi (kwa Ulaya Magharibi na nchi nyingine),zimechaguliwa.

Russia katika kundi la Ulaya Mashariki na Peru katika Kundi la Amerika ya Kusini na Karibiani zimeshindwa kuchaguliwa. Russia imeshindwa kupata kura 97 zinazohitajika kuchaguliwa, huku Peru, ikiwa na kura 108 za ndiyo, imezidiwa na nchi wagombea wengine watatu katika kundi hilo.

Wagombea katika makundi ya Afrika, Asia-Pasifiki, Ulaya Magharibi na mataifa mengine walishinda kirahisi kwani hawakuwa na washindani.

China, Cote d'Ivoire, Cuba, Ufaransa na Malawi zimechaguliwa tena kwa mara nyingine.

Nchi kumi zitaondoka katika Baraza la Haki za Binadamu kufikia mwisho wa mwaka huu ambazo ni Gabon, Senegal (kwa Afrika); Nepal, Pakistani, Uzebekistan (kwa Asia-Pasifiki); Jamhuri ya Czech, Ukraine (kwa Ulaya Mashariki); Bolivia, Mexico (kwa Amerika ya Kusini na Karibiani); Uingereza (kwa Ulaya Magharibi na nchi nyingine).

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lenye makao yake mjini Geneva ni chombo kati ya serikali duniani chenye jukumu la kuhimiza na kulinda haki za binadamu duniani kote. Takriban theluthi moja ya wajumbe wake 47 hubadilishwa kila mwaka ili wajumbe wa baraza hilo watumikie kwa vipindi tofauti vya miaka mitatu kwa ajili ya mwendelezo.

Viti vya nchi wajumbe wa baraza hilo vinagawanywa kwa msingi wa kuwakilisha makundi ya nchi za kanda tofauti: 13 kila moja kwa Afrika na Asia-Pasifiki; 8 kwa Amerika ya Kusini na Karibiani; 7 kwa Ulaya Magharibi na nchi nyingine; 6 kwa Ulaya Mashariki. 

Uchaguzi wa nchi wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ukifanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 10, 2023. (Loey Felipe/Picha Ya UN/ Xinhua)

Uchaguzi wa nchi wajumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ukifanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Oktoba 10, 2023. (Loey Felipe/Picha Ya UN/ Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha