Waziri Mkuu Abiy wa Ethiopia aeleza mafanikio ya BRI kwa Afrika, atoa wito wa hatua jumuishi kujenga uhimilivu

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 19, 2023

(Picha inatoka Xinhua.)

(Picha inatoka Xinhua.)

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) limekuwa na mafanikio mengi kwa Bara la Afrika hasa katika ujenzi wa miundombinu ambayo imesaidia kukua kwa biashara barani Afrika na pia ametoa wito wa kuwepo kwa hatua jumuishi katika kujenga uhimilivu wa kiuchumi.

Akitoa yake hotuba siku ya Jumatano Oktoba 18 kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Viongozi wa Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, Abiy amesema kuwa pendekezo hilo limekuwa na mafanikio katika ujenzi wa miundombinu ambayo imesaidia kuboresha biashara ndani ya Bara la Afrika na China, muunganisho na ukuaji endelevu wa kiuchumi na kijamii, kutoa fursa za ajira kwa wenyeji hali ambayo imeboresha maisha ya watu, kuwezesha mabadilishano ya watu, ujuzi na teknolojia na zaidi limekuwa mbadala wa chanzo cha mtaji kwa ajili ya uwekezaji barani Afrika.

Abeiy ametoa mfano wa reli ya kwanza ya kisasa ya Afrika ya kuvuka mpaka ya Ethiopia-Djibouti ambayo imejengwa chini ya BRI ambapo imekuwa na mchango mkubwa katika huduma za uchukuzi na usafiri wa watu, ongezeko la mnyororo wa thamani wa biashara pembezoni mwa reli, kuwezesha kuongezeka kwa biashara ya ndani na ya nje ya Ethiopia na pia kuifanya Ethiopia kuwa lango la kibiashara katika Pembe ya Afrika kwa kuunganisha Afrika, Mashariki ya Kati na Asia ya mbali.

Amesema, uhusiano kati ya China na Afrika unaanzia miaka zaidi ya 2000 iliyopita ambapo enzi za kiutawala za China ya kale ikiwemo Enzi ya Ming ilikuwa na ushirikiano pia uhusiano wa karibu wa kibiashara kupita Njia ya Kale ya Hariri. Amesema, tangu kipindi hicho China imedumisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Afrika.

Katika hotuba yake hiyo, Abiy pia amepongeza juhudi za Rais wa China Xi Jinping za kuja na mapendekezo ya ustaarabu, usalama na maendeleo ya Dunia ambayo kwa pamoja yanajenga Jumuiya ya Binadamu yenye Mustakabali wa Pamoja. Pia amegusia mipango aliyotangazwa na Rais Xi kwenye mkutano wa viongozi wa China na Afrika uliofanyika hivi karibuni Afrika Kusini ambapo China iliahidi kusaidiana na Bara la Afrika katika kuendeleza sekta ya viwanda, kujenga kilimo cha kisasa na kukuza vipaji vya Afrika katika sekta mbalimbali.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha