Hotuba Kuu Kamili ya Rais Xi Jinping katika Mkutano wa Baraza la 3 la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 19, 2023

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ametoa hotuba kuu kwenye Mkutano wa Baraza la 3 la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja siku ya Jumatano.

Ifuatayo ni hotuba kuu kamili ya Rais Xi:

Kujenga Dunia yenye Uwazi, Jumuishi na Iliyounganishwa Kwa Maendeleo ya Pamoja

Hotuba Kuu ya Mheshimiwa Xi Jinping

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China

Kwenye Ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la 3 la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja

Oktoba 18, 2023

Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali,

Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa,

Wawakilishi wa nchi mbalimbali,

Wageni Waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Marafiki,

Leo, tunakutana hapa kwa ajili ya kufunguliwa kwa Mkutano wa Baraza la 3 la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRF). Kwa niaba ya serikali ya China na watu wa China na kwa jina langu mwenyewe, napenda kuwakaribisha nyote kwa furaha kubwa!

Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 10 tangu kutolewa kwa Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) nililopendekeza. BRI, ikipata hamasa kutoka Njia ya Kale ya Hariri na ikijikita katika kuimarisha mafungamano ya mawasiliano, inalenga kuimarisha sera, miundombinu, biashara, fedha na maelewano kati ya watu, kuingiza msukumo mpya katika uchumi wa dunia, kutoa fursa mpya za maendeleo ya kimataifa, na kujenga jukwaa jipya la ushirikiano wa kimataifa wa kiuchumi.

Katika miaka hii 10 iliyopita, tumeendelea kujitolea kwa dhamira hii anzilishi. Shukrani kwa juhudi zetu za pamoja, ushirikiano wa kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja umeimarika, umekua kwa haraka na kutoa matokeo yenye manufaa.

Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja umeenea kutoka Bara la Ulaya na Asia, Eurasia hadi Afrika na Amerika Kusini. Nchi zaidi ya 150 na mashirika zaidi ya 30 ya kimataifa yametia saini nyaraka za ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja. Tumefanya mikutano miwili ya BRF hapo awali, na tumeanzisha majukwaa zaidi ya 20 maalumu ya ushirikiano wa kimataifa chini ya BRI.

Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja umeendelea kutoka "kuandika muhtasari" hadi "kujaza maelezo," na mipango imegeuzwa kuwa miradi halisi. Idadi kubwa ya miradi alama na programu "ndogo lakini makini" zenye kujikita kwa watu zimeanzishwa.

Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja umepanuka kutoka muunganisho unaoonekana kwa macho hadi muunganisho wa kitaasisi. Kanuni muhimu elekezi za ushirikiano wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja zimewekwa, ambazo ni pamoja na kanuni ya "kupanga pamoja, kujenga pamoja, na kunufaika pamoja," dhana ya ushirikiano wa uwazi, kijani na safi, na lengo la kufuata ushirikiano wa kiwango cha juu, unaojikita kwa watu na endelevu.

Katika miaka hiyo 10 iliyopita, tumejitahidi kujenga mtandao wa kimataifa unaojumuisha kanda za kiuchumi, njia za kimataifa za usafirishaji na njia kuu ya mafungamano ya mawasiliano ya habari inayojumuisha reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, mabomba na gridi za umeme. Huku ukifikia ardhi, bahari, anga na intaneti, mtandao huu umeongeza mzunguko mkubwa wa bidhaa, mitaji, teknolojia na rasilimali watu kati ya nchi zinazohusika na kuingiza nguvu mpya kwenye Njia ya Kale ya Hariri yenye historia ndefu ya miaka elfu moja katika zama mpya.

Treni zinazoendeshwa kwa kasi kwenye njia za reli, magari yanayokimbia barabarani, safari za ndege zinazounganisha nchi mbalimbali, meli za mizigo zinazopasua mawimbi, na biashara ya mtandaoni inayoleta urahisi kwa watu – vyote kwa pamoja vimekuwa alama za biashara ya kimataifa katika zama mpya, kama vile tu misafara ya ngamia na meli zilivyokuwa katika zama zilizopita.

Vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati za maji, upepo na jua, mabomba ya mafuta na gesi, na mitandao ya usambazaji umeme inayozidi kuwa ya teknolojia za kisasa na iliyounganishwa inaondoa kizuizi cha maendeleo kinachosababishwa na uhaba wa nishati na kutimiza ndoto ya nchi zinazoendelea kufikia maendeleo ya kijani na yenye kutoa kaboni chache. Miradi hii ya nishati imekuwa chemchemi na kinara cha maendeleo endelevu katika zama mpya.

Viwanja vya ndege na bandari mpya kabisa, barabara zenye ufanisi, na maeneo mapya maalum ya viwanda yaliyojengwa kwa ajili ya ushirikiano wa kibiashara vimeunda njia mpya za kiuchumi na vichocheo vipya vya ukuaji wa uchumi, na vimekuwa njia za biashara na vituo vya majukwaa kwa zama mpya.

Miaka tajiri na ya kupendeza ya kitamaduni, matamasha ya sanaa, maonyesho, Karakana za Luban, mipango ya mawasiliano kati ya watu kama vile Mpango wa Ujenzi wa Jamii ya Njia ya Hariri na mpango wa Kivitendo wa Mwangaza, na kuongeza mawasiliano kati ya mashirika yasiyo ya kiserikali, jumuiya za washauri mabingwa, mashirika ya vyombo vya habari, na vijana -- shughuli zote hizi zinazostawi zimeunda wimbo wa urafiki katika zama mpya.

Janga la UVIKO-19 lilipotokea, Ukanda Mmoja, Njia Moja ikawa njia ya kuokoa uhai wa maisha. China ilitoa zaidi ya barakoa bilioni 10 na dozi bilioni 2.3 za chanjo kwa nchi nyingine na kuzalisha chanjo kwa pamoja na nchi zaidi ya 20, ikitoa mchango maalum kwa juhudi za nchi washirika wa BRI katika kupambana na UVIKO-19. Na China pia ilipata msaada muhimu kutoka kwa nchi zaidi ya 70 wakati ilipoathiriwa sana na janga hilo.

Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja unatokana na kanuni ya "kupanga pamoja, kujenga pamoja, na kunufaika pamoja." Unavuka tofauti kati ya ustaarabu, tamaduni, mifumo ya kijamii, na hatua za maendeleo. Umefungua njia mpya ya mawasiliano kati ya nchi na nchi, na kuanzisha mfumo kazi mpya wa ushirikiano wa kimataifa. Hakika, BRI inawakilisha utafutaji wa pamoja wa binadamu wa maendeleo kwa wote.

Mabibi na mabwana,

Marafiki,

Mafanikio yetu katika muongo mmoja uliopita ni ya ajabu kweli, na kuna mengi tunayoweza kupata kutoka kwayo.

Tumejifunza kwamba binadamu ni wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja. China inaweza kufanya vizuri pale tu ambapo Dunia inafanya vizuri. China ikifanya vyema, Dunia itakuwa bora zaidi. Kupitia ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, China inafungua mlango wake kwa Dunia hata zaidi, huku maeneo yake ya bara yakibadilika kutoka "beki wa nyuma" hadi kuwa "wachezaji wa mbele," na maeneo ya pwani yakiongeza jitihada mpya katika ufunguaji wao wa mlango. Soko la China limeunganishwa hata kwa karibu zaidi na soko la kimataifa. China imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa nchi na maeneo zaidi ya 140 na chanzo kikuu cha uwekezaji kwa nchi nyingi zaidi. Uwekezaji wa China nje ya nchi na uwekezaji wa kigeni nchini China umeongeza urafiki, ushirikiano, kujiamini na matumaini.

Tumejifunza kwamba ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote ndiyo njia ya uhakika ya kufaulu kuanzisha mipango mikuu ambayo inawanufaisha wote. Nchi zinapokumbatia ushirikiano na kutenda kwa pamoja, genge kubwa linaweza kugeuzwa kuwa njia ya kupita, nchi zisizo na ufikiaji wa bahari zinaweza kuunganishwa na ardhi, na mahali penye maendeleo duni panaweza kugeuzwa kuwa penye ustawi. Nchi zinazoongoza katika maendeleo ya kiuchumi zinapaswa kutoa uungaji mkono kwa washirika wao ambao bado hawajafanikiwa. Sote tunapaswa kuchukuliana kama marafiki na washirika, kuheshimiana na kuungana mkono, na kusaidiana ili kufanikiwa. Kama msemo unavyosema, unapowapa wengine waridi, harufu yao hubaki mkononi mwako. Kwa maneno mengine, kusaidia wengine pia ni kusaidia wewe mwenyewe. Kuona maendeleo ya wengine kuwa tishio au kutegemeana kiuchumi kuwa hatari hakutafanya maisha binafsi kuwa bora zaidi au kuharakisha maendeleo yake.

Tumejifunza kwamba misingi ya Njia ya Hariri ya amani na ushirikiano, uwazi na ujumuishi, kufundishana na kunufaishana ndiyo chanzo muhimu zaidi cha nguvu kwa ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja. Niliwahi kusema kwamba waanzilishi wa njia za kale za hariri wamepata sehemu yao katika historia si kama wavamizi na watekaji kwa meli za kivita, bunduki, farasi au panga. Badala yake, wanakumbukwa kuwa wajumbe wa kirafiki walioongoza misafara ya ngamia na meli zilizobeba mizigo ya bidhaa. Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja unatokana na imani kwamba miali ya moto huwaka zaidi wakati kila mtu anapoongeza kuni kwenye moto na kwamba kusaidiana kunaweza kutufikisha mbali. Ushirikiano wa namna hiyo unalenga kutoa maisha mazuri siyo tu kwa watu wa nchi moja, bali pia kwa watu wa nchi nyingine pia. Unakuza mafungamano ya mawasiliano, kufanya ushirikiano wa kunufaishana, na kutafuta maendeleo kwa pamoja. Mapambano ya kiitikadi, ushindani wa siasa za kijiografia na siasa za kambi siyo chaguo kwetu. Tunachopinga ni vikwazo vya upande mmoja, umwamba wa kiuchumi na kutengana kiuchumi na usumbufu wa minyororo ya usambazaji.

Yale ambayo yamepatikana katika miaka 10 iliyopita yanadhihirisha kuwa ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja uko upande sahihi wa historia. Unawakilisha usongaji mbele wa nyakati zetu, na ni njia sahihi katika kusonga mbele. Tunahitaji kuendelea kuwa macho wazi na bila kutatizwa katika Dunia yenye changamoto, na tunahitaji kufahamu vyema wajibu wetu kwa historia, kwa watu na kwa Dunia. Tunapaswa kukabiliana kwa pamoja na hatari na changamoto mbalimbali za kimataifa, ili kuleta mustakabali mzuri wa amani, maendeleo, ushirikiano na kunufaishana kwa vizazi vijavyo.

Mabibi na mabwana,

Marafiki,

Mabadiliko yanayotokea Dunia katika nyakati zetu, na yenye umuhimu wa kihistoria ni makubwa kuliko ilivyowahi kushuhudiwa. China inajitahidi kujijenga kuwa nchi yenye nguvu zaidi na kustawisha Taifa la China katika sekta zote kwa kufuata maendeleo ya kisasa ya China. Maendeleo ya kisasa tunayoyafuata si kwa China pekee, bali ni kwa nchi zote zinazoendelea kupitia juhudi zetu za pamoja. Maendeleo ya kisasa ya kimataifa yanapaswa kutafutwa ili kuimarisha maendeleo ya amani na ushirikiano wa kunufaishana na kuleta ustawi kwa wote. Tukiwa njiani kusonga mbele, tutakumbana na upepo wa kusukuma nyuma na upepo wa kusukuma mbele tunahitaji kuendelea kulenga lengo letu, kuchukua hatua zenye kuleta matokeo, kuvumilia, na kuendelea kusonga mbele hadi lengo letu litimie. China itafanya kazi pamoja na pande zote zinazohusika katika kuimarisha uhusiano wa ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, kupeleka ushirikiano huu katika hatua mpya ya maendeleo yenye ubora wa juu, na kufanya juhudi zisizo na kikomo za kufikia maendeleo ya kisasa kwa nchi zote.

Sasa, niko tayari kutangaza hatua nane kuu ambazo China itachukua ili kuunga mkono utafutaji wetu wa pamoja wa ushirikiano wa kiwango cha juu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja.

Kwanza, kujenga mtandao wa mafungano ya mawasiliano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja wenye pande nyingi. China itaharakisha maendeleo yenye ubora wa hali ya juu wa Njia ya reli ya mwendokasi ya China-Ulaya, kushiriki katika ukanda wa kimataifa wa usafirishaji wa Caspian, kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Ushirikiano wa Njia ya reli ya mwendokasi ya China-Ulaya, na kufanya juhudi za pamoja za kujenga ukanda mpya wa usafirishaji katika mabara ya Ulaya na Asia, Eurasia uliounganishwa na reli na barabara ya moja kwa moja ya usafirishaji. Tutaunganisha kwa nguvu zote bandari, huduma za usafirishaji na biashara chini ya "Njia ya Hariri ya Baharini," na kuharakisha ujenzi wa Ukanda Mpya wa Kimataifa wa Biashara wa Nchikavu na Baharini na Njia ya Angani ya Hariri.

Pili, kuunga mkono uchumi wa dunia ulio wa uwazi. China itaanzisha maeneo ya majaribio ya ushirikiano wa biashara ya mtandaoni wa njia ya hariri, kuingia mikataba ya biashara huria na mikataba ya ulinzi wa uwekezaji na nchi nyingi zaidi. Tutaondoa vizuizi vyote vya upatikanaji wa uwekezaji wa kigeni katika sekta ya viwanda. Kwa kutilia maanani sheria za kimataifa za uchumi na biashara za viwango vya juu, tutaendeleza zaidi ufunguaji mlango wa kiwango cha juu katika biashara ya huduma za mipakani na uwekezaji, kupanua ufikiaji wa soko kwa bidhaa za kidijitali na nyinginezo, na kuimarisha mageuzi katika maeneo yakiwemo kampuni za serikali, uchumi wa kidijitali, haki miliki za ubunifu na manunuzi ya serikali. China itaendesha Maonyesho ya Biashara ya Kidijitali Duniani kila mwaka. Katika miaka mitano ijayo (2024-2028), jumla ya biashara ya bidhaa na huduma ya China inatarajiwa kuzidi dola trilioni 32 na dola trilioni 5 mtawalia.

Tatu, kufanya ushirikiano wa kivitendo. China itahimiza miradi alama na programu "ndogo lakini makini" za kuhusu maisha ya watu. Benki ya Maendeleo ya China na Benki ya Uuzaji na Uingizaji Bidhaa ya China (China Exim) kila moja itaanzisha dirisha la ufadhili la RMB bilioni 350. Nyongeza ya RMB bilioni 80 itaingizwa kwenye Mfuko wa Njia ya Hariri. Kwa pamoja, fedha hizo zitasaidia miradi ya BRI kwa misingi ya soko na uendeshaji wa biashara. Mikataba ya Ushirikiano yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 97.2 imehitimishwa katika Jukwaa la BRI la Wakurugenzi Watendaji lililofanyika wakati wa mkutano huu. China itatekeleza miradi 1,000 ya usaidizi wa maisha ya watu, na kuimarisha ushirikiano wa elimu ya ufundi wa kazi kupitia Karakana za Luban na mipango mingineyo. Pia tutaongeza juhudi za pamoja ili kuhakikisha usalama wa miradi ya BRI na wafanyakazi wanaohusika.

Nne, kuhimiza maendeleo ya kijani. China itaendelea kuimarisha ushirikiano katika ujenzi wa miundombinu unaotilia maanani ulinzi wa mazingira ya asili, nishati safi na usafirishaji unaojikita katika kuhifadhi mazingira, na kuongeza uungaji mkono kwa Muungano wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kijani ya BRI. China itaendelea kuandaa Mkutano wa Uvumbuzi wa Kijani wa BRI, na kuanzisha mfumo wa mazungumzo na mawasiliano katika ujenzi wa sekta ya photovoltaic na mtandao wa wataalam wa maendeleo ya kijani na yenye kutoa kaboni chache. China itatekeleza Kanuni za Uwekezaji wa Kijani kwa Ukanda Mmoja, Njia Moja, na kutoa fursa za mafunzo 100,000 kwa nchi washirika ifikapo Mwaka 2030.

Tano, kuendeleza uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia. China itaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Ushirikiano katika Uvumbuzi wa Sayansi na Teknolojia wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, kufanya Mkutano wa kwanza wa Ukanda Mmoja, Njia Moja wa kubadilishana uzoefu wa kisayansi na kiteknolojia, kuongeza idadi ya maabara za pamoja zilizojengwa na pande nyingine hadi kufikia 100 katika miaka mitano ijayo, na kusaidia wanasayansi vijana kutoka nchi nyingine kufanya kazi kwa muda mfupi nchini China. Katika jukwaa hili, China itaweka mbele Pendekezo la Usimamizi wa Teknolojia za Akili Bandia (AI) duniani. Tuko tayari kuongeza mawasiliano na mazungumzo na nchi nyingine na kuhimiza kwa pamoja maendeleo mazuri, yenye utaratibu na salama ya AI duniani.

Sita, kuunga mkono mawasiliano ya kiraia. China itaanzisha Jukwaa la Liangzhu ili kuimarisha mazungumzo kuhusu ustaarabu na nchi washirika wa BRI. Mbali na Ligi ya Majumba ya Kimataifa ya Maonyesho ya Njia ya Hariri, Tamasha la Sanaa la Kimataifa la Njia ya Hariri, Muungano wa Kimataifa wa Makumbusho wa Njia ya Hariri, Muungano wa Kimataifa wa Makumbusho ya Sanaa wa Njia ya Hariri, na Muungano wa Kimataifa wa Maktaba wa Njia ya Hariri ambao umeanzishwa, China pia imeanzisha Muungano wa Kimataifa wa Utalii wa Miji ya Njia ya Hariri. Na tutaendelea na Mpango wa ufadhili wa masomo wa Njia ya Hariri wa serikali ya China.

Saba, kuhimiza ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja wenye msingi wa uadilifu. Pamoja na washirika wake wa ushirikiano, China itatoa “Mafanikio na Matarajio ya Ujenzi wenye Uadilifu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja” na “Kanuni za Ngazi ya Juu za Ujenzi wenye Uadilifu wa Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na kuanzisha mfumo wa kutathmini uadilifu na ufuataji taratibu kwa kampuni zinazohusika katika ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja. Pia tutafanya kazi pamoja na mashirika ya kimataifa katika utafiti na mafunzo juu ya kuongeza uadilifu katika ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja.

Nane, kuimarisha ujenzi wa kitaasisi kwa ushirikiano wa kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja. China itashirikiana na nchi washirika wa BRI kuimarisha ujenzi wa majukwaa ya ushirikiano wa pande nyingi yanayohusu nishati, kodi, ufadhili wa kifedha, maendeleo ya kijani, kupunguza maafa, kupambana na ufisadi, washauri mabingwa, vyombo vya habari, utamaduni na nyanja nyinginezo. China itaendelea kuwa mwenyeji wa BRF na kuanzisha sekretarieti ya Baraza hilo.

Mabibi na mabwana,

Marafiki,

Muongo mmoja uliopita imekuwa safari ya ushirikiano wa kujitolea na matokeo yenye manufaa. Ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja ulipendekezwa na China, lakini matunda na fursa zake ni kwa ajili ya Dunia kugawana. Hebu tufikie matarajio ya watu, tubebe majukumu mazito tuliyokabidhiwa na historia, tufuate kwa karibu mwenendo wa nyakati, na tusonge mbele kwa nguvu na kwa kushikamana. Hebu tuimarishe ushirikiano wa kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, na tulete ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja kwenye hatua mpya ya maendeleo yenye ubora zaidi na wa kiwango cha juu. Hebu tuendeleze maendeleo ya kisasa ya nchi zote, tujenge Dunia iliyo ya uwazi, jumuishi na iliyounganishwa kwa ajili ya maendeleo ya pamoja, na tujenge kwa pamoja jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Nautakia mafanikio kamili Mkutano wa Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja!

Asante.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha