

Lugha Nyingine
Rais wa Marekani Joe Biden asaini amri ya kiutendaji juu ya kushughulikia hatari za AI
Rais wa Marekani Joe Biden akitia saini amri ya kiutendaji katika Ikulu ya Marekani, White House mjini Washington, D.C. Oktoba 30, 2023. (Picha na Aaron Schwartz/Xinhua)
WASHINGTON - Rais Joe Biden wa Marekani amesaini amri ya kiutendaji inayolenga kuweka vigezo vya matumizi salama na vya kiusalama kwa ajili ya uendelezaji wa Teknolojia za Akili Bandia (AI) na kushughulikia hatari za teknolojia hiyo mpya.
"Amri ya Kiutendaji inaweka vigezo vipya vya matumizi salama na vya kiusalama vya AI, inalinda faragha ya Wamarekani, inahimiza usawa na haki za kiraia, inaunga mkono upande wa watumiaji na wafanyakazi, inahimiza uvumbuzi na ushindani, inaendeleza uongozi wa Marekani kote duniani, na kadhalika," taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House siku ya Jumatatu imesema.
Amri hiyo inawataka "watengenezaji wa mifumo yenye nguvu zaidi ya AI" kushirikishana na serikali ya Marekani matokeo yao ya majaribio ya usalama na taarifa nyingine muhimu kabla ya kutolewa kwa umma.
Amri hiyo ambayo Biden ameitia saini katika Ikulu ya White House, pia inaelekeza mashirika ya serikali kuweka vigezo vya majaribio hayo na kushughulikia mambo yanayohusiana na hatari za kikemikali, kibaolojia, radiolojia, nyuklia na usalama wa mtandao.
Amri hiyo pia imetoa wajibu na majukumu kwa wizara, idara na mashirika mbalimbali ya Serikali ya Marekani katika kudhibiti na kuratibu mwenendo wa uvumbuzi na matumizi ya teknolojia hizo ikiwa ni pamoja na masuala ya haki miliki za uvumbuzi, hataza, mifumo ya kisheria na kikanuni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma