

Lugha Nyingine
Tasnia ya maonyesho ya China yaimarika tena kwa nguvu katika robo tatu za kwanza za Mwaka 2023
Picha hii iliyopigwa Novemba 2, 2023 ikionyesha banda la Eneo Maalum la Viwanda vya uchumi wa Data la Kimataifa lililoandaliwa kwa ajili ya Maonyesho ya 6 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa kutoka nje ya China (CIIE) mjini Shanghai, Mashariki mwa China, Novemba 2, 2023. (Xinhua/Wang Xiang)
BEIJING – Tasnia ya maonyesho ya China imeimarika tena kwa nguvu katika robo tatu za kwanza za mwaka huu, ikisukumwa na mahitaji makubwa ya soko, Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China Shu Jueting amesema Alhamisi huku takwimu zikionyesha kuwa maonyesho zaidi ya 3,248 yamekwishafanyika kuanzia Januari hadi Septemba ambayo ni ongezeko la asilimia 32.4 kuliko kipindi kama hicho Mwaka 2019.
"Sekta ya maonyesho ni jukwaa muhimu la kujenga mfumo wa kisasa wa soko na mfumo wa kiuchumi ulio wazi," Shu amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Kuhusu Maonyesho ya 6 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa kutoka nje ya China (CIIE), ambayo yamepangwa kufanyika mjini Shanghai kuanzia Novemba 5 hadi 10, Shu amesema wageni kutoka nchi, maeneo na mashirika ya kimataifa 154 watakusanyika katika maonyesho hayo.
Kampuni zaidi ya 3,400 na watembeleaji maonyesho wa kitaaluma karibu 410,000 pia wamejiandikisha kuhudhuria maonyesho hayo.
Ukubwa wa jumla wa eneo la maonyesho ya biashara utafikia mita za mraba 367,000, ikizidi maonyesho yaliyopita, na idadi kubwa inayovunja rekodi ya Kampuni 500 bora duniani na kampuni zinazoongoza katika tasnia zimejipanga kuhudhuria maonyesho hayo, msemaji huyo amesema.
Katika Baraza la Uchumi la Kimataifa la Hongqiao la mwaka huu, ambalo ni sehemu muhimu ya CIIE, Ripoti ya Uwazi ya dunia Mwaka 2023 na Fahirisi mpya ya Uwazi Duniani zitatolewa.
Shughuli zaidi 1,000 kama vile mikutano ya jopo kwa kampuni za kigeni pia zitafanyika wakati wa maonyesho hayo, msemaji huyo amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma