Chuo Kikuu cha Addis Ababa chasaini makubaliano ya ushirikiano wa ufadhili wa masomo na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 06, 2023

Wageni wakiwa katika picha za pamoja baada ya hafla ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa ufadhili wa masomo mjini Addis Ababa, Ethiopia, Novemba 3, 2023. (Picha na Misikir Temesgen/Xinhua)

Wageni wakiwa katika picha za pamoja baada ya hafla ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa ufadhili wa masomo mjini Addis Ababa, Ethiopia, Novemba 3, 2023. (Picha na Misikir Temesgen/Xinhua)

ADDIS ABABA - Wawakilishi wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa (AAU) na Ubalozi wa China nchini Ethiopia siku ya Ijumaa zimetia saini makubaliano ya ushirikiano wa ufadhili wa masomo na China ili kuongeza ubora wa elimu ambayo yatashuhudia serikali ya China kutoa fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi zaidi ya 120 wa shahada ya kwanza na ya baada ya shahada ya kwanza kutoka AAU katika kipindi cha mwaka mmoja.

"Idadi kubwa ya wanafunzi watafaidika kutokana na makubaliano haya. Ni mpango wa aina yake wenye manufaa mengi kwa Chuo Kikuu cha Addis Ababa," Samson Mekonnen, Makamu Mkuu wa Chuo wa Mawasiliano ya Kimkakati na Mambo ya Kimataifa wa AAU, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuchangia katika jitihada mpya za AAU kikiwa ni chuo kikuu cha kwanza kabisa cha umma cha kujitegemea katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Akihudhuria hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo, Balozi wa China nchini Ethiopia Zhao Zhiyuan amebainisha kuwa Taasisi ya Confucius imekuwepo katika AAU tangu Mwaka 2013, ikitoa huduma bora za ufundishaji wa lugha ya Kichina kwa jamii za wenyeji.

“Mbali na hilo, Ubalozi wa China mwaka jana ulianzisha fursa maalum za ufadhili wa masomo katika AAU ili kusaidia miradi ya kitaaluma na utafiti ya wanafunzi,” Zhao amesema, na kuongeza kuwa ubalozi pia umehimiza programu za mabadilishano ya wanafunzi na wafanyakazi, utafiti wa pamoja kati ya AAU na vyuo vikuu vya China, vilevile ushirikiano kati ya kampuni za China na AAU kuhusu kuajiri wahitimu.

"Ubalozi wa China unathamini sana ushirikiano na AAU. Tutaunga mkono AAU na vyuo vikuu vya China katika kujenga uhusiano. Tunawakaribisha walimu na wanafunzi kutoka chuo kikuu hiki kutembelea na kusoma nchini China ili kuharakisha mawasiliano katika maendeleo na ustaarabu," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha