Majira ya baridi kali yaleta athari Kaskazini mwa China, na hatua za dharura zachukuliwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 07, 2023

Wafanyakazi wa usafi wa mazingira wakiondoa theluji kutoka barabarani huko Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, Kaskazini Mashariki mwa China, Novemba 6, 2023. (Xinhua/Wang Jianwei)

Wafanyakazi wa usafi wa mazingira wakiondoa theluji kutoka barabarani huko Harbin, Mkoa wa Heilongjiang, Kaskazini Mashariki mwa China, Novemba 6, 2023. (Xinhua/Wang Jianwei)

BEIJING - Huku utabiri wa halijoto ya usiku ukishuka hadi nyuzi joto sifuri, Mji Mkuu wa China, Beijing umeanza usambazaji wake wa joto siku ya Jumatatu ikiwa ni wiki moja mapema kuliko wakati uliopangwa huku baridi kali ikisababisha upepo mkali na theluji kubwa mikoa ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa China tangu Jumapili.

Kwa kukabiliana na hali hizo, serikali za mitaa zimechukua hatua za dharura, ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kwa muda kwa masomo na shughuli za biashara, pamoja na kuwasha mapema mifumo ya joto.

Mkoa wa kaskazini zaidi wa Heilongjiang umetoa tahadhari nyekundu siku ya Jumapili kwa vimbunga vya theluji, kwa mujibu wa idara ya huduma ya hali ya hewa ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa utabiri, miji mingi katika mkoa huo ilikuwa ikitarajiwa kukumbwa na theluji kubwa, huku jumla ya theluji hiyo ikikadiriwa kuwa kati ya 20 mm na 40 mm, kuanzia Jumapili jioni hadi jana Jumatatu jioni.

Wimbi hilo la baridi lilikuwa likitarajiwa kuleta vimbunga na theluji katika mikoa ya Heilongjiang, Jilin, na Liaoning pamoja na Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya Ndani kuanzia Jumapili asubuhi hadi Jumatatu jioni, kwa mujibu wa Kituo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha China.

"Duru hii ya theluji inatarajiwa kuwa kubwa sana, haswa Kusini Mashariki mwa Mkoa wa Heilongjiang, ambapo mvua na theluji inaweza kuzidi rekodi za kihistoria za wakati huu wa mwaka uliopita," Fang Chong, Mtabiri Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha China amesema.

Siku ya Jumatatu, Harbin, Mji Mkuu wa Heilongjiang, ulisimamisha huduma za usafiri wa abiria na kusimamisha masomo yote mjini humo.

Wakati huo huo, theluji kubwa ilisababisha kufungwa kwa shule katika miji mbalimbali ya mikoa ya Liaoning na Jilin siku ya Jumatatu.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Taiping mjini Harbin uliendelea kufanya kazi siku ya Jumatatu, lakini ulitangaza kufuta safari 39 za ndege.

Ili kukabiliana na hali hiyo ngumu ya hewa, mikoa ya kaskazini-mashariki ya China imeitikia upesi dharura zinazohusiana na theluji, na kuongeza juhudi za kudumisha utulivu na kuhakikisha usalama.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha