Rais Xi atoa wito wa kusukuma uhusiano kati ya China na Ufaransa kwenye ngazi mpya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 21, 2023

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Jumatatu katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron ametoa wito wa kuendeleza urafiki wa jadi kati ya China na Ufaransa na kusukuma uhusiano huo katika ngazi mpya.

Huku akieleza kuwa Mwaka 2024 ni maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, na baada ya ziara ya Macron nchini China Mwezi Aprili mwaka huu, matokeo mengi yamepatikana katika mawasiliano ya ngazi tofauti na ushirikiano kwenye sekta mbalimbali. Rais Xi amesema China iko tayari kudumisha mawasiliano ya ngazi ya juu na Ufaransa, na kufanikisha mkutano ujao wa mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya China na Ufaransa kuhusu mawasiliano ya kiutamaduni, kusukuma maendeleo mapya katika ushirikiano wa nchi hizo mbili katika maeneo kama vile elimu, utamaduni na utafiti wa kisayansi, na kuhimiza mawasiliano ya kirafiki kati ya watu wa nchi hizo mbili.

Akipongeza ushiriki wa Ufaransa katika Mkutano wa viongozi wa Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Maonyesho ya 6 ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China, Rais Xi amesema China inafurahi kuona bidhaa za Ufaransa zinaongezeka katika soko la China na inakaribisha uwekezaji zaidi wa kampuni za Ufaransa nchini China.

Rais Xi amesema China iko tayari kuimarisha ushirikiano na Ufaransa katika Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.

Akisisitiza kwamba China na Ufaransa zimedumisha ushirikiano mzuri kuhusu mabadiliko ya Tabianchi, Rais Xi amesema Mkutano wa 28 wa Nchi Watia saini (COP28) kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi huko Dubai utajikita kwa mara ya kwanza katika Makubaliano ya Paris, kufanya majumisho na kutathmini maendeleo ya utekelezaji wake, na kuongoza mchakato wa siku zijazo wa uongozi wa masuala ya tabianchi duniani.

Amesema China na Umoja wa Ulaya zinapaswa kubaki washirika wa ushirikiano wa kunufaishana katika dunia yenye hali ya utatanishi na iliyofungamana na anatumai kuwa Ufaransa itachukua jukumu la kiujenzi katika kuhimiza maendeleo chanya ya uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya.

Kwa upande wake Macron amesema kuwa ziara yake ya mafanikio nchini China Mwezi Aprili mwaka huu bado imo katika kumbukumbu yake, na kwamba ameridhishwa na mawasiliano na majadiliano ya hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili katika ngazi zote.

Amesema, Ufaransa inatarajia kuwasiliana kwa karibu na China juu ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabia Nchi huko Dubai na kuendelea kushirikiana kushughulikia masuala ya kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa viumbe anuai.

Wakibadilishana mawazo kuhusu mgogoro wa Palestina na Israel, wakuu hao wa nchi wamesema ni muhimu kuepusha hali isizidi kuwa mbaya kati ya Palestsina na Israel , hasa kuibuka kwa msukosuko mkubwa zaidi wa ubinadamu.

Wamekubaliana kuwa suluhisho la “nchi mbili” ndiyo njia ya kimsingi ya kutatua mzunguko wa migogoro ya Palestina na Israeli.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha