

Lugha Nyingine
Mwanariadha wa Kenya aweka rekodi mpya ya Mbio za Marathon za Shanghai
Bingwa wa Mbio za Marathon za Shanghai 2023 kwa upande wa wanaume Philimon Kiptoo Kipchumba akivuka mstari wa mwisho wa mbio tarehe 26, Novemba 2023. (Picha/CFP)
Mwanariadha wa Kenya Philimon Kiptoo Kipchumba ameweka rekodi mpya kwenye Mbio za Marathon za Shanghai kwa upande wa wanaume baada ya kumaliza mbio hizo kwa kutumia saa mbili, dakika 5 na sekunde 35 katika shughuli hiyo iliyofanyika Jumapili mjini Shanghai, China.
Muda wake huo umevunja rekodi iliyopita, iliyowekwa na Paul Lonyangata, mwanariadha mwenzake kutoka Kenya ambaye alimaliza mbio hizo za umbali wa kilomita 42.195 kwa kutumia saa 2 dakika 7 na sekunde 14 mwaka 2015.
“Hali ya hewa ilikuwa nzuri leo. Nimeweza kuona watu wengi wakinitia hamasa. Mwishowe, ilikuwa ni ushindani mkali, kwa hivyo nilijitahidi kukimbia kwa haraka katika kilomita ya 42, na hivyo ndivyo namna nilivyoweza kunyakua ubingwa,” amesema Kipchumba.
Alphonce Felix Simbu kutoka Tanzania amemaliza mbio hizo sekunde 4 tu nyuma ya mshindi huyo, akishinda nafasi ya pili.
Kwa mujibu wa waandalizi, asilimia 12 hivi ya washiriki 38,000 wa mbio hizo za mwaka 2023 wanatoka ng’ambo. Na kati ya washiriki wa China, zaidi ya 10,000 wametoka nje ya Shanghai.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma