

Lugha Nyingine
Kundi la Hamas lawaachilia huru kundi la tatu la mateka, majadiliano ya kuongeza muda wa kusimamisha vita yaendelea
![]() |
Mfungwa wa Kipalestina (kushoto) akirudi Jerusalem baada ya kuachiliwa huru kutoka Gereza la Ofer la Israel, Novemba 24, 2023. (Muammar Awad/Xinhua) |
GAZA - Kikosi cha Al-Qassam, ambacho ni tawi la wanamgambo wenye silaha la Kundi la Hamas, limeawaachilia huru kundi la tatu la mateka siku ya Jumapili kutoka Ukanda wa Gaza chini ya makubaliano ya kusimamisha vita kati yake na Israel ambapo Jeshi la Israel limethibitisha katika taarifa kwamba limepokea mateka 13 wa Israel kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu, wakiwemo wanawake wanne na watoto tisa, huku mtoto mdogo zaidi akiwa na umri wa miaka minne.
"Katika mfumo kazi wa mapatano ya kusimamisha vita kibinadamu, tumekabidhi kwa Shirika la Msalaba Mwekundu mateka 13 wa Israel, watatu ni raia wa Thailand na raia mmoja wa Urusi," Al-Qassam imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Redio ya Jeshi la Israel imesema sehemu ya mchakato wa makabidhiano hayo ulifanyika Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na kuongeza kuwa "mateka kadhaa walivuka mpaka kutoka sehemu kati ya Gaza na Israel."
Jeshi hilo limeeleza kuwa "wahudumu wa Msalaba Mwekundu walikabidhi mateka 12 kwa Kikosi Maalumu cha Jeshi la Israel na shirika la usalama wa ndani la Israel, Shin Bet kwenye uzio wa mpaka wa Ukanda wa kati wa Gaza, ambao watawasafirisha hadi Kituo cha Kijeshi cha Hatzerim."
Limeongeza kuwa mateka wa 13, ambaye ni mwanamke mwenye umri wa miaka 84 anayeugua ugonjwa, amesafirishwa moja kwa moja kwa ndege hadi Hospitali ya Soroka katika mji wa Beer Sheva, Kusini mwa Israel.
Wakati huo huo, idara ya wafungwa ya Shirika la Ukombozi wa Palestina imechapisha orodha ya wafungwa 39 wa Kipalestina walioachiliwa huru Jumapili jioni, wakiwemo 21 kutoka Jerusalem, mmoja kutoka Ukanda wa Gaza, na wengine kutoka Ukingo wa Magharibi.
Mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la China, Xinhua aliyepo Ramallah amethibitisha kuwasili kwa mabasi yaliyowasafirisha wafungwa 39 wa Kipalestina walioachiwa huru, ambao wote ni watoto.
"Qatar na Misri zimewasilisha rasimu ya makubaliano kwa Israel na Hamas juu ya kuongeza muda wa kusimamisha vita unaotarajiwa kumalizika Jumatatu na kuwezesha mabadilishano ya wafungwa wengi zaidi kati ya pande hizo mbili zinazopigana," chanzo cha habari ambacho hakikutaka kuwekwa wazi kimeliambia Xinhua.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema katika taarifa yake ya video siku ya Jumapili kwamba anaweza kukubali kuongeza muda wa kusimamisha vita kwa siku chache ikiwa Hamas itawaachilia mateka zaidi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma