Simulizi ya Kocha wa sarakasi wa Kenya kuhusu historia yake ya sarakasi na China yaonesha uhusiano wa kina wa urafiki

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 28, 2023

(Picha imechukuliwa kutoka video ya ChinaDaily.)

Mathias Kavita akiwa kwenye ofisi yake mjini Nairobi. (Picha imechukuliwa kutoka video ya tovuti ya ChinaDaily)

Mathias Kavita, kocha wa kiwango cha juu wa sarakasi wa Kenya hakutarajia kuwa safari yake ya kwenda China miaka 40 iliyopita itabadilisha maisha yake kwa njia ya kushangaza.

Kavita kutoka Mombasa, kipindi hicho akiwa na miaka 13 hakuwa akijua chochote kuhusu sarakasi mpaka alipotazama filamu ya sarakasi pamoja na vijana wenzake 23 kwenye Ubalozi wa China mjini Nairobi. Wakati huo Kavita pia akiwa ni mchezaji wa mazoezi ya viungo vya mwili, alikuwa ndiyo tu amemaliza kushinda ubingwa wa mashindano ya kitaifa.

“Kabla ya kusafiri China, tulipokea mafunzo ya utangulizi, ambayo yalihusisha kutazama filamu za sarakasi zilizorekodiwa China,” amesema Kavita kwenye ofisi yake ya Nairobi, ambayo imetapakaa vifaa vya sarakasi, miongoni mwao viliagizwa kutoka China.

Amesema, “Nikiwa ni mchezaji wa mazoezi ya viungo kipindi hicho, filamu ya sarakasi tuliyotazama kwenye Ubalozi wa China, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuweza kutazama maonesho ya namna hiyo. Nilivutiwa hasa na watoto wa China wakionyesha vitendo ambavyo nilikuwa sijawahi kuona kabla.”

“Hili lilinifanya niwe na nia thabiti zaidi kusafiri China na kujifunza zaidi.”

Kavita sasa anafanya kazi na shirika la “Sarakasi Trust” kuibua vipaji vya sarakasi vya vijana, akiwa amefundisha wanasarakasi zaidi ya 1,000 wanaotumbuiza kwenye maonyesho Duniani kote.

“Mafunzo yangu nchini China yalikuwa muhimu sana, kwa sababu yamenifanya niwe mwanasarakasi wa kimataifa na mwalimu mzuri wa sarakasi,” amesema.

Eric Musyoka, mmoja kati ya wanasarakasi waliofundishwa na Kavita amemsifu sana kocha huyu na mafunzo yake. “Kocha Mathias alikuwa ni mtu kwa kwanza kunionesha namna ya kufanya sarakasi. Alisema siku moja utakuja kutambua kwamba kile unachokifanya sasa hivi kitakupelekea mahali ambapo hujawahi kufika. Nikasema, ngoja nijaribu...Nimekwenda Hispania, sikuweza kuamini hadi nilipokuwa nimekaa ndani ya ndege!”

“Hapa Kenya sarakasi ni yenye manufaa kwa vijana kama sisi. Mara tu ukiwa mwanasarakasi utajidhibiti kinidhamu na utajua ni mambo gani ufanye. Haina maana katika maisha yako, kama utakuwa mwizi au kuanza kujihusisha na dawa za kulevya,” amesema Musyoka.

Hata baadhi ya wanasarakasi wanaofanya sarakasi zao mitaani katika barabara za Nairobi waliwahi kufundishwa na Kavita. Mwanasarakasi Alexsander amesema, “Mathias alinifundisha namna ya kuwa shupavu. Alitambua kwamba nilikuwa na kipaji na alikuja kunichagua kutoka mitaani. Huu ni mwaka wangu wa tano tangu niondoke mtaani. Ninafurahi sana. Kuishi Nairobi bila familia kwakweli ni kama msongo wa mawazo. Marafiki zangu wengi wamejiua. Wamekuwa wakijihusisha na dawa za kulevya. Wamekufa. Lakini nimekuwa shupavu siku zote hizi. Kwa sababu bado nina mustakabali.”

“Wanasarakasi kama wale wanaofanya maonyesho mitaani kwenye kando za barabara wana ujasiri huo na nia ya kujifunza. Kama tunaweza kupata shule kama ile tuliyojifunza huko Guangzhou (nchini China), tutaweza kuokoa maisha ya watu wengi mtaani,” amesema Kavita.

Mwezi Oktoba mwaka huu, timu ya Kavita iliandaa maonesho ya sarakasi mjini Nairobi, ambayo yalichanganya ngoma ya Kiafrika, dansi ya kisasa na mtindo wa sarakasi. “Tunajitahidi kubuni mambo mapya kila wakati tukifanya maonesho. Katika maonesho yote haya, sehemu ya kimsingi ni ujuzi wote ambao tulijifunza China. Kuna mguso wa Kichina ndani yake muda wote,” amesem Kavita.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha