Waziri wa Mambo ya Nje wa China ahimiza utekelezaji kamili wa maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 01, 2023

UMOJA WA MATAIFA - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi siku ya Jumatano kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York alipokutana na waandishi wa habari baada ya kuongoza mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Palestina na Israel ametoa wito wa kutekeleza kikamilifu maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu suala la Palestina na kurudi kwenye njia sahihi ya suluhu ya nchi mbili.

Huku akieleza kuwa duru mpya ya mgogoro kati ya Palestina na Israel imesababisha vifo vingi vya raia na maafa makubwa ya kibinadamu, Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema jumuiya ya kimataifa inatarajia Baraza la Usalama kutekeleza wajibu wake ipasavyo na kuchukua hatua kali.

“Ikiwa nchi mwenyekiti wa zamu wa Baraza la Usalama kwa mwezi wa Novemba, China daima imekuwa ikichukulia mgogoro kati ya Palestina na Israel kama suala muhimu zaidi,” Wang amesema.

Amesema baada ya kupitishwa kwa azimio namba 2712, ambalo ni azimio la kwanza la Baraza la Usalama tangu kuzuka kwa mgogoro huo, chini ya uenyekiti wa China, China imeitisha mkutano wa ngazi ya juu wa Jumatano kuitikia wito mkali wa jumuiya ya kimataifa.

Amesema, mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka nchi karibu 20 wameshiriki katika mkutano huo. Washiriki wamefanya majadiliano ya kina kuhusu hali ya sasa ya Palestina na Israel na hatua zinazofuata, wakijenga maelewano zaidi na kuunganisha nguvu kwa ajili ya kurejesha amani.

"Tunakaribisha usimamishaji vita wa kibinadamu uliofikiwa wiki iliyopita. Lakini amani haiwezi kuzuiliwa na hakupaswi kuwa na kikomo cha muda wa kusimamisha mapigano. Dirisha la fursa likifunguliwa, halipaswi kufungwa tena. Mapigano yakisimamishwa, hayapaswi kupamba moto tena. Hatuwezi kuruhusu maafa ya kibinadamu kuendelea au kuvumilia mateso au hasara zaidi miongoni mwa raia," amesema huku akitoa wito kuachiliwa kwa wale wote waliotekwa nyara na kuondolewa kwa hali ya kudhibitiwa kwa Gaza.

Ameeleza kuwa, mgogoro kati ya Palestina na Israel unathibitisha kwa mara nyingine tena kwamba suluhu ya nchi mbili ndiyo njia pekee inayowezekana kutatua suala la Palestina.

Amesema, miaka zaidi ya 70 imepita na vizazi vya Wapalestina vimepoteza makaazi yao na kulazimika kuhama kwenye ardhi yao. Hata hivyo, ndoto ya kuanzisha nchi huru ya Palestina bado haijatimizwa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha