

Lugha Nyingine
Mwanadiplomasia Mwandamizi wa China Wang Yi aomboleza kifo cha Kissinger
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, akitembelea Ubalozi wa Marekani nchini China kuomboleza kifo cha Henry Kissinger aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Desemba 5, 2023. (Xinhua/Shen Hong)
Beijing - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi Jumanne alikwenda kwenye Ubalozi wa Marekani nchini China kuomboleza kifo cha Henry Kissinger aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ambapo ameandika katika kitabu cha maombolezo na kutoa salamu za dhati za rambirambi kwa kuondokewa na Dkt Kissinger.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, ameeleza kuwa Dk. Kissinger ni rafiki wa watu wa China tangu zamani, na watu wa China watakumbuka mchango wake wa kihistoria kwa ajili ya kuanzishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Marekani.
"Muda umethibitisha na utaendelea kuthibitisha kwamba uamuzi wa kisiasa uliofanywa na Dk. Kissinger na viongozi wa China wa wakati huo unaendana na masilahi ya kimsingi ya watu wa pande mbili, mwelekeo wa nyakati, na matarajio ya Jumuiya ya Kimataifa." amesema.
Wang amesema, Dk. Kissinger siku zote alikuwa akifuatilia maendeleo ya China kwa mtazamo wa kirafiki na kufuata hali halisi ilivyo. Aliamini kabisa kwamba China na Marekani, zikiwa ni nchi mbili kubwa, zinapaswa na lazima ziishi pamoja kwa amani.
Alikuwa na uwezo wa kutafuta muafaka wa pamoja na fursa za ushirikiano kutoka katika tofauti kati ya nchi hizo mbili, akionyesha maono na ufahamu wake kama mwanadiplomasia, mwanamkakati na mwanasiasa.
Amesisitiza kuwa wakuu wa nchi hizo mbili walikuwa na mkutano wenye mafanikio mjini San Francisco, walifanya mawasiliano ya kina kuhusu masuala ya kimkakati, masuala ya mambo ya jumla na ya kimsingi kuhusu uhusiano kati ya China na Marekani, na kufikia mfululizo wa maafikiano muhimu, ambayo yatasaidia kuboresha na kuendeleza uhusiano baina ya nchi hizo katika mwelekeo mzuri, thabiti na endelevu. Amezitaka pande hizo mbili kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na wakuu hao wa nchi.
Wang ameeleza matumaini yake kuwa upande wa Marekani utashirikiana na China, kufanya juhudi zaidi ili kuimarisha maelewano na ushirikiano, na kuchukua vitendo halisi ili kudumisha mwelekeo tulivu na uboreshaji wa uhusiano kati ya China na Marekani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma