Somalia yaungana na tume ya FAO kudhibiti nzige wa jangwani

(CRI Online) Desemba 07, 2023

Somalia imejiunga na Tume ya Kudhibiti Nzige wa Jangwani katika Kanda ya Kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) siku ya Jumatano na kuwa nchi mwanachama wake wa 17.

FAO imesema Somalia imepata maendeleo makubwa ya kujenga uwezo wa kitaasisi na kiufundi wa kudhibiti nzige tangu Mwaka 2020 kwa msaada kutoka kwa wakala na washirika wa chakula wa Umoja wa Mataifa.

Kiongozi wa Tume ya FAO inayoshughulikia tatizo la Nzige na Wadudu wengine waharibifu wa mimea na Magonjwa yanayovuka mipaka, Shoki AlDobai, amesema Somalia ni nchi muhimu ya kuzaliana kwa nzige, na kuwa nao katika Tume hiyo kutanufaisha siyo Somalia tu bali nchi jirani pia kwa kuimarisha ufuatiliaji na kutoa tahadhari ya mapema kwenye kanda hiyo.

Kwa mujibu wa FAO, eneo la kijiografia la Somalia, umuhimu wa kihistoria katika udhibiti wa nzige na michango kwa Tume inaifanya kuwa mhusika muhimu katika kupambana na nzige katika Pembe ya Afrika.

Imesema uanachama wa Somalia katika Tume hiyo ni hatua ya kimkakati itakayosaidia kuboresha juhudi za kudhibiti nzige kwenye kanda hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha