Rais wa Tanzania Samia akagua eneo lililokumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi, huku idadi ya vifo ikiongezeka hadi 76

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 08, 2023

Katesh baada ya mvua mkubwa tarehe 5, Desemba, 2023.

Picha iliyopigwa tarehe 5, Desemba, 2023 ikionesha Mji wa Katesh baada ya mvua mkubwa. (Picha/VCG)

DAR ES SALAAM - Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesafiri kwenda Mkoa wa Manyara, kaskazini mwa nchi hiyo na kukagua uharibifu uliosababishwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika Wilaya ya Hanang mkoani humo siku ya Jumapili.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia maafa, Jenista Mhagama, akitoa ripoti kwa Rais amesema, idadi ya waliofariki katika mafuriko hayo ya Desemba 3 imeongezeka hadi 76 kutoka idadi ya Jumatano ya watu 69, na kuongeza kuwa mafuriko hayo yamesababisha watu zaidi ya 5,600 kukosa nyumba za kuishi, na mashamba ya mazao zaidi ya 750 yameharibiwa na mifugo mingi kuuawa.

“Watu takriban 440 kati ya 5,600 waliokosa nyumba za kuishi wanakaa kwenye sehemu tatu za kujihifadhi kwa muda shuleni huku wengine wakikaa na ndugu,” amesema Mhagama.

Timu ya maafisa 1,285 kutoka idara za ulinzi na usalama walikuwa wakiendelea kutafuta miili zaidi, ameongeza.

"Serikali itawatimizia gharama za matibabu, chakula, na mahitaji mengine muhimu katika safari yenu ya kurejea maisha ya kawaida," Rais Samia amewahakikishia waathirika baada ya kukagua eneo lililokumbwa na maafa hayo na kutembelea wagonjwa waliolazwa hospitalini, na wale wanaokaa kwenye makazi ya kujihifadhi kwa muda.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Mji wa Katesh ambao ni moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi, Rais Samia amewataka wakazi wa Mkoa wa Manyara kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu ambacho kinaweza kusababishwa na kuathirika kutokana na hali mbaya ya utoaji wa maji baada ya vyanzo vya maji kuharibika.

Pia ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyoathirika.

“Pia nimeagiza wizara zinazohusika kupeleka maafisa wa ushauri nasaha ili kusaidia watu walioathiriwa na maafa kupata nafuu,” amesema mkuu huyo wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Katesh, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanazania na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Mobhare Matinyi amesema, maafa hayo hayakusababishwa na mlipuko wa volcano, na ameondoa uwezekano wa kutokea kwa mlipuko wa volcano kwa mujibu wa uchunguzi waliofanya wataalamu wa jiolojia wa Wizara ya Madini na Idara ya Uchunguzi wa Jiolojia ya Tanzania (GST).

Kwa mujibu wa wataalamu hao, miamba kwenye milima ya Hanang ilizidiwa na maji mengi yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha maporomoko hayo ya udongo na tope.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha