

Lugha Nyingine
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa aonya kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya DRC na Rwanda
Bintou Keita (Kulia, mbele), mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 11, 2023. (Eskinder Debebe/Picha ya UN / Xinhua)
NEW YORK - Mjumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Bintou Keita, ameonya juu ya uwezekano wa kuongezeka kwa mvutano kati ya DRC na Rwanda akisema kuwa hali katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC imezidi kuwa mbaya Mwezi Disemba na kwamba mvutano kati ya DRC na Rwanda umeongezeka zaidi, na kuongeza hatari ya mapigano ya moja kwa moja ya kijeshi ambayo yanaweza kuiingiza Burundi.
Mvutano kati ya DRC na Rwanda ni mkubwa sana na hatari ya kuongezeka kwa mapigano ya kijeshi kati yao bado ni kubwa licha ya juhudi za kikanda na kimataifa za kupunguza hali ya wasiwasi, amesema katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Jumatatu.
Nchi hizo mbili zinashutumiana kuunga mkono makundi yenye silaha Mashariki mwa DRC na matukio ya kuvuka mpaka yameongezeka, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama kuhusu hali ya DRC.
Hali ya usalama, huduma na haki za binadamu imezorota kusini mwa Jimbo la Kivu Kaskazini, Mashariki mwa DRC, hasa kufuatia kuanza tena kwa mapigano kati ya Jeshi la DRC na waasi wa M23 Mwezi Oktoba, na mashambulizi ya M23 katika eneo la Masisi katika jimbo hilo kufuatiakuanza kuondolewa kwa askari wa Kikosi cha Kijeshi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kutokana na ombi la serikali ya DRC, mamlaka ya Kikosi cha Kijeshi cha EAC hayakuongezwa muda wake ilipofika Desemba 8 na kikosi hicho kimeanza kuondoka. Wakati huo huo, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afŕika (SADC) inajiandaa kutuma kikosi kipya nchini DRC katika wiki zijazo.
"Juhudi hizi za kikanda zinastahili kupongezwa. Hata hivyo, hazitaweza kufikia malengo yake bila uwekezaji endelevu na wa kudumu wa serikali ya DRC katika michakato ya kisiasa ya kikanda, kitaifa na ya ndani kwa ajili ya kutatua migogoro mashariki mwa nchi," amesema Keita.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likifanya mkutano kuhusu hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 11, 2023. (Eskinder Debebe/Picha ya UN / Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma