

Lugha Nyingine
China yafanya kumbukumbu ya kitaifa kwa wahanga wa mauaji makubwa ya Nanjing
China ikifanya hafla ya 10 ya kitaifa ya kumbukumbu ya wahanga wa Mauaji Makubwa ya Nanjing kwenye Jumba la Kumbukumbu za Wahanga wa Mauaji Makubwa ya Nanjing yaliyofanywa na wavamizi wa Japan mjini Nanjing, mji mkuu wa Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Desemba 13, 2023. (Xinhua/Ji Chunpeng)
NANJING - Licha ya baridi kali, maelfu ya watu, wakiwa wamevalia mavazi meusi na maua meupe kifuani, wamehudhuria hafla ya 10 ya kumbukumbu ya kitaifa ya wahanga 300,000 wa Mauaji Makubwa ya Nanjing huko Nanjing, Mkoa wa Jiangsu nchini China ambapo watu walisimama kimya na ving'ora vilisikika kote mjini humo wakati China ilipofanya hafla hiyo ya kumbukumbu siku ya Jumatano.
Bendera ya Taifa la China ilipeperushwa nusu mlingoti mbele ya umati wa watu wakiwa pamoja na watu walionusurika katika mauaji makubwa, wanafunzi wanaosoma Nanjing na marafiki wa kigeni.
Saa 4:01 asubuhi (kwa saa za China), ving'ora vilianza kulia. Madereva katika eneo la katikati ya mji huo walisimamisha magari yao na kupiga honi, huku watembea kwa miguu wakisimama kimya kuwakumbuka wahanga.
Li Hongzhong, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Naibu Spika wa Bunge la Umma la China, alishiriki kwenye hafla hiyo ya kumbukumbu na kutoa hotuba.
Amesema, hafla hiyo ya kumbukumbu inaonyesha nia kuu ya watu wa China ya kutafuta maendeleo ya amani kwa uthabiti na inaonyesha msimamo wao thabiti wa kukumbuka historia kila wakati, kuthamini amani na kusonga mbele kwa mustakabali mwema.
Vijana zaidi ya 80 walisoma kwa sauti tamko la amani, na wajumbe wa raia walipiga Kengele ya Amani. Njiwa weupe wanaoashiria tumaini la amani waliachiliwa kuruka juu ya uwanja wa Jumba la Kumbukumbu ya Wahanga wa Mauaji Makubwa ya Nanjing yaliyofanywa na wavamizi wa Japan.
Mwaka 2014, Bunge la Umma la China liliamua Desemba 13 kuwa siku ya kumbukumbu ya kitaifa ya wahanga wa Mauaji Makubwa ya Nanjing, ambayo yalifanyika wakati wanajeshi wa Japan walipokalia mji huo Desemba 13, 1937. Wavamizi wa Japan waliwaua kikatili raia na askari wa China wasiokuwa na silaha takriban 300,000 katika muda wa zaidi ya wiki sita, hili lilikuwa moja ya matukio ya kinyama zaidi ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia (WWII).
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma