Marais wa China na Kenya zabadilishana salamu za pongezi kwa kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 15, 2023

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Kenya William Ruto wametumiana salamu za pongezi kwa kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili. Rais Xi amesema tangu kuanzishwa kwa uhusiano huo miaka 60 iliyopita, China na Kenya zimekuwa zikishirikiana na kusukuma mbele maendeleo bega kwa bega, akiongeza kuwa nchi hizo mbili zimekuwa marafiki wa kuaminiana kisiasa na washirika wazuri katika ushirikiano wa kunufaishana wa kiuchumi.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi hizo mbili zimeshuhudia mabadilishano ya mara kwa mara ya viongozi wa ngazi za juu, hali ya kuaminiana kisiasa inayozidi na kupata matokeo makubwa chini ya ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, Rais Xi amesema, huku akisisitiza kuwa pande hizo mbili ziko mstari wa mbele katika ushirikiano kati ya China na Afrika, siyo tu katika kunufaisha watu wa pande hizo mbili, lakini pia kutoa mfano wa kuigwa kwa ushirikiano wa China na Afrika.

Rais Xi ameeleza kuwa wakati Rais Ruto alipohudhuria Mkutano wa 3 wa Baraza la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja mjini Beijing mwezi Oktoba, yeye na Ruto walifikia makubaliano muhimu kuhusu maendeleo ya baadaye ya uhusiano wa pande mbili.

Rais Xi amesema yuko tayari kushirkiana na Rais Ruto kuchukua maadhimisho hayo ya kutimia miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kama mwanzo mpya, kuanzisha njia ya ushirikiano wenye umaalumu wenyewe katika safari ya maendeleo na ustawishaji ya kila upande.

Katika ujumbe wake, Ruto amesema tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi miaka 60 iliyopita, Kenya na China zimeshirikiana na kukabiliana mabadiliko ya hali ya kimataifa, na kutilia maanani kuheshimiana, kuungana mkono, kufanya ushirikiano wa kirafiki, kushikamana na kusaidiana huku ushirikiano wao ukizidi kuwa na nguvu zaidi.

“Ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili na mabadilishano ya kitamaduni yameleta matokeo mazuri,” Ruto amesema huku akiongeza Kenya iko tayari kujiunga na China kufuatilia matokeo ya Mkutano wa 3 wa Baraza la Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja na Mazungumzo ya Viongozi wa China na Afrika mjini Johannesburg ili uhusiano wa pande hizo mbili ukumbatie mustakabali mzuri wa maendeleo endelevu, ustawi, urafiki na maendeleo ya pamoja.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha