Mji wa Beijing, China waendesha huduma ya majaribio ya mabasi ya shule yanayotumia Umeme

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 15, 2023

Wanafunzi wa shule ya msingi No.1 katika eneo la Fengtai la Beijing wakishuka kutoka kwenye basi la shule lililoundwa maalum kwa ajili ya shule hiyo hapa Beijing, Septemba 1, 2023. (Xinhua/Ju Huanzong)

Wanafunzi wa shule ya msingi No.1 katika eneo la Fengtai la Beijing wakishuka kutoka kwenye basi la shule lililoundwa maalum kwa ajili ya shule hiyo hapa Beijing, Septemba 1, 2023. (Xinhua/Ju Huanzong)

Akikaribisha mwanga wa jua la asubuhi, Chen Jiaqi mwenye umri wa miaka 10 kutoka eneo la Haidian la Beijing alitembea mwenyewe hadi kwenye kituo cha mabasi kilichopo karibu na nyumbani kwao. Baada ya basi la shule la kijani linalotumia umeme kufika, mhudumu wa kujitolea alishuka kwa ajili ya kupakia wanafunzi waliopo huku Chen akipanda basi hilo na kulipa nauli kwa kutumia kadi yake ya malipo.

“Wazazi wangu walikuwa wakiendesha gari kunipeleka shuleni, lakini ilikuwa inakera kukwama kwenye foleni ya magari njiani kuelekea shuleni na hasa karibu na lango la shule,” amesema Chen, huku akiongeza kuwa basi la shule linaunganisha nyumbani kwao na shuleni bila kusimama kwenye foleni, kwa kuwa basi hilo hupita kwenye njia maalum kwa ajili ya mabasi.

Ili kuhudumia wanafunzi wanaopokea elimu ya lazima, Beijing ilianza kufanya majaribio ya kutoa huduma hiyo ya mabasi ya shule katika maeneo manne mwezi wa Septemba. Idadi ya shule zinazohusika na mradi huo imeongezeka hadi zaidi ya 20 kutoka 13 za awali, huku idadi ya abiria kwa wastani kila siku ikiongezeka kutoka 811 hadi zaidi ya 4,000.

Kundi la kwanza la mabasi 100 ya shule yote yameanza kufanya kazi, yakiwa na sifa ya uendelevu, amesema Zhao Zhen kutoka Idara ya Usafiri ya Beijing.

“Kila safari na mabasi haya ni hatua moja kuelekea sayari ya kijani zaidi,” amesema Zhao, huku akiongeza kuwa kwa mabasi hayo kutumia nishati ya umeme, mji wa Beijing unapiga hatua katika ahadi yake ya kupunguza utoaji wa kaboni.

Hatua hiyo pia inakuja kama suluhisho la maendeleo endelevu ya jiji hilo, ambalo linakabiliana na foleni kubwa za magari. Kwa mujibu wa idara ya usafiri ya mji huo, shule zinazofanya majaribio hayo ya mabasi zimeshuhudia kupungua kwa magari binafsi ya kuchukua na kupeleka wanafunzi kwa asilimia 12.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi No.1 katika eneo la Fengtai wakiwa kwenye basi la shule lililotengenezwa maalum kwa ajili ya shule hiyo hapa Beijing, Septemba 1, 2023. (Xinhua/Ju Huanzong)

Wanafunzi wa Shule ya Msingi No.1 katika eneo la Fengtai wakiwa kwenye basi la shule lililotengenezwa maalum kwa ajili ya shule hiyo hapa Beijing, Septemba 1, 2023. (Xinhua/Ju Huanzong)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha