Sisi wa Misri ashinda uchaguzi wa urais kwa asilimia 89.6 ya kura zote halali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 19, 2023

Picha hii iliyopigwa Desemba 18, 2023 ikionyesha mkutano na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa urais mjini Cairo, Misri. (Xinhua/Wang Dongzhen)

Picha hii iliyopigwa Desemba 18, 2023 ikionyesha mkutano na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa urais mjini Cairo, Misri. (Xinhua/Wang Dongzhen)

CAIRO - Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uchaguzi ya Kitaifa ya Misri (NEA) Hazem Badawy ametangaza Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari mjini Cairo kwamba Rais aliye madarakani Abdel-Fattah al-Sisi ameshinda uchaguzi wa urais wa Mwaka 2024 kwa kupata kura milioni takriban 40, sawa na asilimia 89.6 ya kura zote halali, huku akisema kuwa raia karibu milioni 44.8 ndani na nje ya nchi hiyo walipiga kura katika uchaguzi huo, kati ya wapiga kura milioni 67 walio na sifa, ikiwa ni sawa asilimia na 66.8, ambayo ni "idadi kubwa zaidi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika historia ya Misri."

Hazem Omar, anayeongoza Chama cha Republican People's, amepata asilimia 4.5 ya kura zote, akifuatiwa na Farid Zahran wa Chama cha Social Democratic cha Misri, na Abdel-Sanad Yamama wa Chama cha Wafd cha Misri.

Kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, Sisi ametoa hotuba kwa watu wa nchi nzima, ambapo amesema "kunichagua kwa safari ya kuongoza nchi ni jukumu ambalo ninabeba kwa uaminifu."

"Nchi inakabiliana na changamoto nyingi katika ngazi zote," ya juu kabisa ni mgogoro wa Gaza ambao unatishia "usalama wa nchi ya Misri," amesema.

"Tuna uwezo wa kijeshi na kiuchumi kwa ajili ya kuhimili ulinzi wa usalama wa nchi na maslahi ya watu," rais huyo wa Misri ameongeza.

Uchaguzi huo wa Misri ulifanyika Desemba 10-12 huku Wamisri walioko ng'ambo wakipiga kura Desemba 1-3 katika nchi 121.

Matokeo hayo ni ya mwisho kwani mgombea aliyeko madarakani ameshinda kwa kura nyingi na kuiepusha nchi hiyo kwenda katika duru ya pili ya uchaguzi, kwa mujibu wa sheria za Misri. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha