

Lugha Nyingine
BioNTech yazindua kiwanda cha kwanza cha kuzalisha chanjo za mRNA nchini Rwanda
Rais wa Rwanda Paul Kagame akitoa hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kwanza cha kutengeneza chanjo za mRNA barani Afrika cha kampuni ya bioteknolojia ya BioNTech, mjini Kigali, Rwanda, Desemba 18, 2023. (Ikulu ya Rwanda/ Xinhua)
KIGALI - BioNTech, kampuni inayoongoza ya bioteknolojia, imezindua kiwanda chake cha kwanza cha kuzalisha chanjo ya mRNA barani Afrika siku ya Jumatatu katika Mji Mkuu wa Rwanda, Kigali ambapo uzinduzi huo umekuja baada ya kampuni hiyo ya Ujerumani kusaini mikataba Mwaka 2021 na Rwanda na Taasisi ya Pasteur de Dakar nchini Senegal kuanzisha maeneo ya kuzalisha chanjo katika bara hilo. Ujenzi wa kiwanda hicho ulizinduliwa mwaka jana.
BioNTech imeeleza katika taarifa yake kwamba iko mbioni kuzalisha chanjo za kukinga magonjwa za mRNA zinazolenga magonjwa ya mlipuko kama vile kifua kikuu, malaria, na VVU, na pia inaangazia magonjwa yanayoweza kuenea sana, ukiwemo wa Mpox.
Kikiwa katika Eneo la Kiuchumi la Rwanda mjini Kigali, kiwanda hicho kinaweza kuzalisha dozi hadi milioni 50 kila mwaka za chanjo ambazo zina mchakato wa RNA sawa na ule wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 ya Pfizer-BioNTech, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), amesema kuzinduliwa kwa kiwanda hicho ni matokeo madhubuti ya nia thabiti ya kisiasa na ushirikiano mzuri. "Bara la Afrika limejitolea kuongeza uwepo wa chanjo na dawa zingine ili zipatikane kwa Waafrika wote." amesema.
Afrika inaagiza kutoka nje asilimia 70 ya dawa zake na kuzalisha asilimia 1 tu ya chanjo zake, kwa mujibu wa takwimu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Rais wa Rwanda Paul Kagame ameuelezea uzinduzi huo kama hatua kubwa kwa Bara la Afrika katika kufikia usawa wa chanjo.
Marais Macky Sall wa Senegal, Nana Akufo-Addo wa Ghana, Waziri Mkuu wa Barbados Mia Amor Mottley pamoja na Ursula von der Leyen, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, walihudhuria uzinduzi huo.
Ursula von der Leyen, Rais wa Kamisheni ya Ulaya akitoa hotuba kwenye hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kwanza cha kutengeneza chanjo za mRNA barani Afrika cha kampuni ya bioteknolojia ya BioNTech, mjini Kigali, Rwanda, Desemba 18, 2023. (Ikulu ya Rwanda/ Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma