

Lugha Nyingine
Uwekezaji wa China wawezesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Malawi
Huu ni mwaka wa 10 tangu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” (BRI) litolewe. Balozi wa Malawi nchini China, Bw. Allan Joseph Chintedza anaona kuwa pendekezo hilo ni mfumo wa kunufaishana na kuwezesha maendeleo ya Malawi.
Balozi Chintedza amesema katika mahojiano maalum ya hivi karibuni na Shirika Kuu la Utangazi la China kwamba, hivi sasa Malawi iko katika mchakato wa mageuzi ya muundo wa uchumi, na ujenzi wa miundombinu unahitajika zaidi, kwani maendeleo hayapatikani bila ya miundombinu bora, lakini gharama za ujenzi wa miundo mbinu ni kubwa.
Amesema, wakati nchi nyingine zinapokwepa uwekezaji katika sekta hiyo, BRI inaweka kipaumbele katika maendeleo ya miundombinu ya nchi zilizojiunga na pendekezo hilo, hali ambayo inaendana na mahitaji ya maendeleo ya Malawi.
Balozi Chintedza ameongeza kuwa, “Miradi Tisa” iliyotangazwa na Rais wa China Xi Jinping katika Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) imerahisisha mchakato wa uuzaji bidhaa za Afrika kwa China, ambapo si tu imesababisha ukuaji wa uchumi jumuishi na maendeleo endelevu barani Afrika, bali pia inakidhi mahitaji ya soko la China, na kunufaisha pande zote mbili.
Balozi Chintedza anaamini kuwa, kutokana na mfumo wa ushirikiano wa kunufaishana wa BRI na FOCAC, ushirikiano wa kibiashara kati ya Malawi na China utaongezeka kwa kiasi kikubwa katika siku zijazo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma