Serikali ya DRC yapinga maandamano yaliyopangwa kufanyika leo mjini Kinshasa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 27, 2023

KINSHASA - Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imepinga kufanyika kwa maandamano makubwa huko Kinshasa, mji mkuu wa nchi hiyo, yaliyopangwa kufanyika leo Jumatano na wagombea kadhaa wa nafasi ya urais wa vyama vya upinzani, amesema Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC, Peter Kazadi siku ya Jumanne.

Wagombea watano wa nafasi ya urais walitangaza wiki iliyopita kuanzisha maandamano makubwa mjini Kinshasa kuanzia leo Jumatano kulaani kukiuka kanuni za kisheria katika mchakato wa uchaguzi wa Desemba 20 wakati wapiga kura nchini DRC walipopiga kura zao kumchagua rais mpya, wajumbe wa Bunge la Taifa na Mabaraza ya Mikoa, pamoja na madiwani wa manispaa.

"Ninawahakikishia, hakutakuwa na maandamano haya. Yanakiuka kanuni ya kisheria ya kupinga matokeo (ya uchaguzi) katika Mahakama ya Katiba," amesema Kazadi kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, akiwa sambamba na msemaji wa serikali Patrick Muyaya.

Upigaji kura uliongezwa muda rasmi hadi siku iliyofuata kwani idadi kubwa ya vituo vya kupigia kura havikuweza kufunguliwa kutokana na kufika kwa kuchelewa kwa zana na vifaa vya kupigia kura. Uongezaji huo wa muda ulielezwa kuwa kinyume cha sheria ya uchaguzi na Katiba ya nchi hiyo.

"Kasoro hizo zinathibitisha vya kutosha kwamba Desemba 20, 2023, ulikuwa uchaguzi wa udanganyifu, ulioandaliwa kinyume na haki ya kimsingi ya watu wa Kongo", kwa mujibu wa taarifa ya wagombea watano wa urais, wakiwemo Martin Fayulu na Denis Mukwege, wagombea wakuu wawili wa wapinzani katika kinyang'anyiro hicho, ambao pia wametaka kufanyika kwa maandamano hayo leo Jumatano.

Serikali imekuwa ikichukua hatua katika ngazi ya jeshi na polisi kulinda amani na usalama katika eneo lote la nchi hiyo. Wananchi wametakiwa kuwa watulivu na kuendelea kufuatilia kwa utulivu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo, amesema Muyaya.

Maandamano hayo yamepangwa kuanzia Triumphal Boulevard, ambapo bunge la nchi hiyo liko karibu kabisa na makao makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI), katikati mwa jiji la Kinshasa. Hadi kufikia sasa, hakuna mgombea yeyote kati ya hao waliotangaza kuanza kwa maandamano hayo ambaye ametoa maoni yake kuhusu kauli za Kazadi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha