

Lugha Nyingine
Mkutano kati ya viongozi wa Jeshi la Sudan na vikosi vya kijeshi vya uasi waahirishwa
KHARTOUM - Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza Jumatano kuahirishwa kwa mkutano kati ya viongozi wa Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na askari wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF), ambao ulikuwa umepangwa kufanyika nchini Djibouti leo Alhamisi.
Wizara hiyo imesema katika taarifa yake kwamba iliarifiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Djibouti, nchi mwenyekiti wa zamu wa Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (IGAD), kwamba Kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo hakuweza kuhudhuria mkutano huo na mkuu wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan uliopangwa kufanyika leo Alhamisi kutokana na sababu za kiufundi.
Kutakuwa na uratibu tena wa kufanya mkutano mwezi Januari mwaka ujao, imeongeza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Al-Burhan, kutokana na nia yake ya kumaliza mateso ya watu wa Sudan yanayosababishwa na "wanamgambo waasi," alikuwa tayari kuondoka Jumatano jioni kwa ajili ya mkutano huo uliopendekezwa na IGAD.
Wizara hiyo imeeleza zaidi masikitiko yake juu ya "mbinu ya kuchelewesha ya RSF na kutokuwa tayari kukomesha uharibifu wa Sudan na kuwadhuru watu."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma