

Lugha Nyingine
China yasaidia watu waliokimbia makazi yao Sudan Kusini
JUBA - Sudan Kusini imesema siku ya Alhamisi kwamba malori yaliyobeba vitu vya msaada wa kibinadamu vilivyotolewa na China kwa wakimbizi na watu wasio na makazi wanaorejea kutoka Sudan yameanza kuwasili Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.
Waziri wa Masuala ya Kibinadamu na Usimamizi wa Majanga Albino Akol Atak amesema malori sita yakiwa na vipande jumla ya 26,145 vya plastiki kwa ajili ya kujenga makazi ya muda yamewasili Juba kusaidia watu waliorejea na wakimbizi.
"Huu ni mchango mkubwa wa serikali ya China kwa watu wa Sudan Kusini na ni matokeo ya mawasiliano yetu na jumuiya ya kimataifa na wafadhili kwa ajili ya wao kuisaidia serikali na kuunga mkono juhudi za serikali katika mwitikio wake wa kuingia kwa wingi kwa wakimbizi na watu wanaorejea ambao wamekuja kutokana na mgogoro nchini Sudan," Akol amewaambia waandishi wa habari mjini Juba.
Amesema watu zaidi ya 460,000 tayari wamekimbia makazi yao hadi Sudan Kusini kutokana na mgogoro huo wa Sudan na wanahitaji makazi, chakula na dawa katika vituo wanakowekwa kwa muda na mahali wanakoenda na kukaa hatimaye.
Akol amesema msaada huo wa China utatumika kuwajengea makazi ya muda watu wanaorejea na wakimbizi katika vituo vya muda na mahali wanakoenda na kukaa hatimaye.
Ameeleza kuwa kutakuwa na vitu vya msaada mwingine vyenye thamani ya dola za Kimarekani jumla ya milioni 1.4 kutoka kwa serikali ya China kwa watu waliokimbia makazi yao, vitu hivyo vya msaada vitawasilishwa kabla ya mwisho wa Januari 2024.
Akol ametoa shukrani kwa mchango wa ukarimu wa serikali ya China, na kusifu urafiki wa kweli kati ya Sudan Kusini na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma