Matetemeko mengi ya ardhi yatikisa katikati mwa Japan, na kusababisha vifo na kukatika kwa huduma za umma

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 02, 2024

Ratiba ikionyesha kucheleweshwa kwa treni kutokana na matetemeko ya ardhi katika Stesheni ya Shinjuku mjini Tokyo, Japan, Januari 1, 2024. (Xinhua/Zhang Xiaoyu)

Ratiba ikionyesha kucheleweshwa kwa treni kutokana na matetemeko ya ardhi katika Stesheni ya Shinjuku mjini Tokyo, Japan, Januari 1, 2024. (Xinhua/Zhang Xiaoyu)

TOKYO - Matetemeko mfululizo ya ardhi yameikumba katikati ya Japan huku tahadhari ya tsunami ikiwa bado inaendelea, na kusababisha angalau watu 13 kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa, kubomoka kwa nyumba, kukatika kwa umeme na kuvurugika kwa utaratibu wa usafiri wakati wa likizo ya Mwaka Mpya.

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japan (JMA), imesema miongoni mwa mfululizo wa matetemeko hayo, tetemeko kubwa zaidi lililofikia kipimo cha richta cha awali cha ukubwa wa 7.6 limetokea saa 10:10 jioni kwa saa za Japan (0710 GMT) kwenye Peninsula ya Noto katika Mkoa wa Ishikawa. JMA imeliita rasmi tetemeko hilo kuwa ni Tetemeko la Ardhi la Noto Peninsula la Mwaka 2024.

Kufuatia kutokea kwa tetemeko hilo, nyumba na barabara zimeporomoka na moto mkubwa ukazuka katika Mkoa wa Ishikawa na maeneo jirani, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Japan.

Maafisa wa wizara ya viwanda ya Japan wamesema takriban kaya 34,000 katika Mikoa ya Ishikawa, Niigata na Toyama hazina umeme kuanzia saa 11:30 jioni kwa saa za Japan siku ya Jumatatu.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema kuwa kazi ya kuwaokoa watu walioathiriwa na matetemeko hayo ya ardhi ni vita dhidi ya wakati, serikali tayari imetuma askari kadhaa wa kikosi cha kujilinda katika maeneo yaliyoathiriwa na wataendelea kutoa msaada.

Tahadhari za Tsunami bado ipo

Matetemeko hayo pia yamesababisha tahadhari za tsunami kwenye pwani ya Bahari ya Japan. Katika maeneo ambayo tahadhari za tsunami zimetolewa, wakaazi wanahamia maeneo ya juu na maeneo mengine ya salama. "Hatujui tsunami itakuja lini, na matetemeko ya baadaye yanatisha," amesema Kai Mawaki, mkazi wa Suzu, mji ulio kwenye ncha ya Peninsula ya Noto.

Kukatika kwa huduma muhimu kwaathiri uokoaji

Kukatika kwa mawasiliano na usafirishaji kumeathiri juhudi za uokoaji katika maeneo yaliyoathiriwa na matetemeko hayo huku barabara na mitambo ya mawasiliano ikiharibika.

Kwa mujibu wa mamlaka ya usafirishaji, njia 40 za treni na njia mbili za huduma ya reli ya mwendo kasi kuelekea eneo lililokumbwa na tetemeko zimesimamisha huduma, huku barabara kuu sita zikifungwa na moja ya kiwanja cha ndege cha Ishikawa ikilazimika kufungwa kutokana na ufa katika njia ya kurukia ndege.

Wasiwasi juu ya vinu vya nyuklia

Wasiwasi juu ya usalama wa vinu vya nyuklia vya Japan (NPPs) umejitokeza kutokana na ajali ya Fukushima. Mamlaka ya Udhibiti wa Nyuklia ya Japan (NRA) siku ya Jumatatu ilisema hakuna dosari zilizopatikana kwenye vinu vya kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia kando ya Bahari ya Japan, ikiwa ni pamoja na vinu vitano vinavyofanya kazi katika mitambo ya Ohi ya Kituo cha Nishati cha Kansai na Kinu cha Takahama katika Mkoa wa Fukui.

Tangu Jumatatu, Japan imekumbwa na matetemeko 155.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha