

Lugha Nyingine
Tume ya Uchaguzi ya DRC yasema Felix Tshisekedi amechaguliwa tena kuwa Rais
Picha hii iliyopigwa Tarehe 31 Desemba, 2023 ikionyesha mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. (Picha na Alain Uyakani/Xinhua)
KINSHASA - Felix Tshisekedi amechaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa muhula wa pili wa miaka mitano, baada ya kupata asilimia 73.34 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 20, huku Moise Katumbi, mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, akishinda nafasi ya pili kwa kupata takriban asilimia 18 ya kura zote, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) imesema Jumapili.
Tume hiyo imetangaza kuwa watu zaidi ya milioni 18, kati ya wapiga kura jumla ya milioni 44 waliojiandikisha, walipiga kura zao.
Rais mteule amepangwa kuapishwa Januari 20, 2024, baada ya Mahakama ya Kikatiba ya DRC kuidhinisha matokeo hayo ya uchaguzi Januari 10.
Uchaguzi huo mkuu uliofanyika Desemba 20 ulishuhudia madai ya ukiukwaji wa taratibu wakati nchi hiyo ya Afrika ya Kati ilipokuwa ikimchagua rais mpya, wajumbe wa Bunge la Taifa na Mabaraza ya Mikoa, pamoja na magavana wa majimbo. Denis Kadima, Mkuu wa CENI, amesema kuwa kasoro zilizoripotiwa wakati wa mchakato wa uchaguzi ni "ndogo" na hazitaathiri matokeo ya uchaguzi.
Kutokana na kuchelewa kufika kwa vitu na vifaa vya kupigia kura, vituo vingi vya kupigia kura havikuweza kufunguliwa kwa wakati, na hivyo kusababisha kuongezwa kwa muda rasmi wa upigaji kura hadi siku iliyofuata. Hata hivyo, baadhi ya wagombea wa urais wanaona muda huu wa nyongeza ni kinyume cha sheria ya uchaguzi na Katiba ya nchi hiyo.
Taarifa ya wagombea watano wa urais, wakiwemo Martin Fayulu na Denis Mukwege, washindani wakubwa katika kinyang'anyiro hicho, ilidai kuwa "kasoro zinathibitisha vya kutosha kwamba uchaguzi uliofanyika Desemba 20, 2023, ulikuwa wa udanganyifu, ulioandaliwa kwa kukiuka haki za kimsingi za watu wa DRC."
Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi na CENI, wagombea kadhaa wa urais wa upinzani siku ya Jumapili waliitisha maandamano makubwa na kutaka uchaguzi ufanyike upya.
Mvutano umekuwa ukiongezeka tangu kuanza kwa upigaji kura, sawa na chaguzi zilizopita. Mwaka 2018, Tshisekedi alichukua madaraka baada ya kushinda uchaguzi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi kukabidhiana madaraka kwa amani nchini humo tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Ubelgiji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma