Rais wa Mpito wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno asema nchi hiyo inaelekea kuwa jamhuri mpya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 02, 2024

YAoundE - Rais wa mpito wa Chad, Mahamat Idriss Deby Itno, amesema kwamba nchi hiyo inaelekea kuwa jamhuri mpya inayozingatia msingi wa uhuru, haki na heshima ya kitaifa baada ya kupitishwa kwa katiba mpya.

Katiba mpya imeleta Jamhuri ya tano, ambayo itaanzisha uwiano mpya wa mamlaka, taasisi zenye nguvu na za kijamhuri na demokrasia ya "kweli ya mashinani" kupitia ugatuaji wa madaraka wenye nguvu, Rais Deby amesema.

"Nimejitolea kuifanya Jamhuri ya tano kuwa Jamhuri yenye nguvu na yenye malengo makubwa, inayokidhi matakwa ya watu wetu na kuendana na hali halisi ya bara linalobadilika kwa kasi," Deby amesema katika hotuba yake kwa taifa siku ya Jumapili usiku.

"Jamhuri hii ya tano itakumbatia kikamilifu mwelekeo wetu, itaendana na asili ya kitamaduni na nyakati zetu, na itajibu matarajio halali ya watu ambao wamekuwa wakiteseka sana. Naahidi kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa ajili ya jamii yenye haki na usawa zaidi,” ameongeza.

Siku ya Alhamisi, Mahakama ya Juu ya Chad ilitangaza kuwa katiba mpya ya nchi hiyo imepitishwa katika kura ya maoni iliyofanyika Desemba 17 kwa asilimia 85.90 ya kura za kuiidhinisha.

Hali ya kisiasa na kijeshi nchini Chad imezorota tangu Mwaka 2021 kufuatia kifo cha Rais wa zamani Idriss Deby Itno. Mahamat Idriss Deby Itno tangu wakati huo amekuwa akiongoza baraza la mpito la kijeshi kutawala nchi hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha