Kenya yatoa dola za Marekani milioni 13.3 kusaidia kaya maskini kutokana na gharama kubwa za maisha

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 03, 2024

NAIROBI - Kenya imesema Jumanne kwamba imetoa shilingi bilioni 2.09 za Kenya (kama dola milioni 13.3 za Kimarekani) ili kusaidia kaya zenye mapato ya chini kutokana na kuzidi kupanda kwa gharama za maisha ambapo kaya takribani milioni 1.04 maskini na zilizo hatarini zitapata msaada wa kifedha kwa ajili ya mahitaji ya mwezi mmoja.

"Mpango wa kutuma pesa moja kwa moja unasaidia wanajamii walio hatarini zaidi kwa kuwapa ruzuku ya kuwaondoa umaskini na njaa, na kuboresha maisha yao," Florence Bore, Waziri wa Wizara ya Kazi na Ulinzi wa Jamii ya Kenya amesema katika taarifa iliyotolewa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Bore ameongeza kuwa wanufaika watapokea fedha hizo kupitia majukwaa ya mtandaoni ya kutuma pesa kwa njia ya simu ili kuongeza urahisi kwa wapokeaji.

Ameeleza kuwa watakaopokea ruzuku hizo ni pamoja na kaya zenye watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, watu wenye hali mbaya ya ulemavu pamoja na wazee.

Aidha, wizara hiyo pia imetoa dola nyingine za Kimarekani 37,725 ili kuimarisha lishe ya kaya maskini nchini humo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha