

Lugha Nyingine
Ethiopia yasema iko tayari kutoa mchango wa kiujenzi ikiwa mwanachama mpya wa BRICS
ADDIS ABABA - Serikali ya Ethiopia imeeleza kuwa iko tayari kutoa mchango wa kiujenzi katika mfumo wa BRICS wakati uanachama wake wa BRICS ukianza rasmi siku ya Jumatatu ambapo katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa siku hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema uanachama wake katika familia ya BRICS, umeonyesha dhamira ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika mfumo wa Ushirikiano wa Kusini-Kusini.
Imesema, uanachama huo pia unatambua mchango mkubwa wa Ethiopia wa pande nyingi katika kuhimiza amani, usalama na ustawi wa kimataifa, pamoja na kuendelea kujitoa na uongozi katika ushirikiano wa Kusini-Kusini.
Wizara hiyo imesema uamuzi huo wa kihistoria wa kuialika Ethiopia kujiunga na mfumo wa BRICS umetambua hali ya sasa na uwezo wa kiuchumi wa Ethiopia ambao unafanyiwa mageuzi.
"Ikiongozwa na kanuni zake za muda mrefu na historia tajiri ya ushirikiano wa pande nyingi, Ethiopia inaendelea kujitoa na iko tayari kutoa mchango wa kiujenzi katika kuhimiza amani na ustawi ikiwa nchi mwanachama mpya wa familia ya BRICS kwa ushirikiano na nchi wanachama wengine," imesema.
Wizara hiyo imesema kamati ya taifa ya mawaziri na kamati andamizi ya uratibu imeanzishwa ili kuhakikisha kuwa Ethiopia inashiriki kikamilifu katika kundi hilo.
BRICS ni kifupi cha mfumo wa ushirikiano nchi zenye masoko yanayoibukia ambao hapo awali ulijumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Kwenye Mkutano wa Kilele wa 15 wa BRICS uliofanyika Mwezi Agosti mjini Johannesburg, Afrika Kusini, nchi zikiwemo Misri, Ethiopia, Iran, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilialikwa kujiunga na kundi hilo. Uanachama wa nchi hizi umeanza rasmi Januari Mosi, 2024.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma