Watu 40 wafariki kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

(CRI Online) Januari 03, 2024

Mvua kubwa iliyonyesha wiki iliyopita mjini Bukavu, Jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), imesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kuua watu takriban 40.

Mamlaka za huko zimesema watu takriban 20 wamepatikana wakiwa wamekufa huko Bukavu na wengine 20 katika kijiji jirani cha Burhinyi. Mamlaka za jimbo hilo zimesema timu za uokoaji zimetumwa kwenye maeneo yaliyoathirika kutafuta waathirika.

Wiki iliyopita, watu takriban 20 walikufa kwenye maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha katika kijiji cha Kalingi katika Wilaya ya Mwenga, Kivu Kusini.

Mwezi Mei 2023, kwenye eneo la Kalehe la Kivu Kusini, miili takriban 438 ilipatikana katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa, na inakadiriwa kuwa watu zaidi ya 5,000 hawakupatikana.

Mafuriko na maporomoko ya ardhi ni ya kawaida nchini DRC wakati wa msimu wa mvua, ambao huanza Septemba hadi Mei, na mara nyingi huwa na athari mbaya.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha