

Lugha Nyingine
Wakimbizi wageuza takataka kuwa hazina katika Kambi ya Wakimbi ya Dukwi nchini Botswana
Mwanamke akionyesha bidhaa ya mapambo iliyotengenezwa na wakimbizi wanawake katika Kambi ya Wakimbizi ya Dukwi, iliyoko umbali wa kilomita takriban 550 Kaskazini Mashariki mwa Gaborone, mji mkuu wa Botswana, Juni 20, 2023. (Picha na Shingirai Madondo/Xinhua)
GABORONE - Katika Kambi ya Wakimbizi ya Dukwi, iliyoko umbali wa takriban kilomita 550 Kaskazini Mashariki mwa Gaborone, mji mkuu wa Botswana, baadhi ya wanawake wamegeuza vitu vilivyotupwa kuwa bidhaa za kupendeza. Evert Mabela, mwenye umri wa miaka 44 aliyekimbia vita Kivu Kaskazini, jimbo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akiamka kabla ya mapambazuko na wenzake huanza shughuli zao za kila siku za kuokota vitu hivyo vilivyotupwa.
Vitu hivi vikiwemo magazeti ya zamani, plastiki na kadibodi vilivyookotwa kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Dukwi, hugeuzwa kuwa bidhaa mbalimbali na kuuzwa ili kuongeza mapato yao.
Kati ya wakimbizi 430 wa DRC wanaoishi katika kambi hiyo, Mabela amevumilia shida kubwa, kupoteza nyumba yake, jamaa na shughuli za kujipatika mapato kutokana na vita katika nchi yake ya asili. Hata hivyo, anaendelea kuwa na nia thabiti ya kuleta mchango chanya kwa jamii na mazingira yake.
"Ninakataa kupoteza matumaini na nimedhamiria kuleta matokeo chanya kwa jamii yangu na mazingira," amesema. Mabela ana imani kwamba kutokana na ahadi za Botswana za kulinda wakimbizi, atafanikiwa.
Kazi zao za mikono wanazobuni, kuanzia fremu za picha na vyungu vya maua hadi mapambo ya mezani na vishikizi vya kalamu, mara nyingi huuzwa kwa bei kati ya dola 5 na 20 za Marekani.
Mabela anakiri kuwa huenda bidhaa zao hazijakamilika vilivyokwa kuwa bado wanaendelea kuboresha ujuzi lakini anasisitiza dhamira yao ya kulinda usafi wa mazingira na kuongeza mapato yao.
Tangu kuanzishwa kwake Aprili 2023, mradi huo umevutia wakimbizi wanawake takriban 30 kutoka nchi mbalimbali katika Kambi ya Wakimbizi ya Dukwi, wote wamejitolea kugeuza takataka kuwa hazina.
Kambi ya Wakimbizi ya Dukwi iliyoanzishwa Mwaka 1978, sasa ina wakimbizi wasiopungua 725, kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na Wizara ya Sheria ya Botswana.
Picha hii, iliyopigwa Juni 20, 2023, ikionyesha baadhi ya bidhaa za mapambo zilizotengenezwa na wakimbizi wanawake katika Kambi ya Wakimbizi ya Dukwi, iliyoko umbali wa kilomita takriban 550 Kaskazini Mashariki mwa Gaborone, mji mkuu wa Botswana. (Picha na Shingirai Madondo/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma