

Lugha Nyingine
Reli ya Jakarta-Bandung nchini Indonesia yabeba abiria zaidi ya 220,000 wakati wa likizo ya mwisho wa mwaka
Abiria wakijipiga picha ndani ya behewa la treni ya mwendo kasi ya EMU inayotoa huduma kwenye Reli ya Mwendokasi ya Jakarta-Bandung nchini Indonesia, Oktoba 17, 2023. (Xinhua/Xu Qin)
JAKARTA - Reli ya Mwendo kasi ya Jakarta-Bandung (HSR), ambayo ni ya kwanza ya aina yake katika eneo la Asia Kusini-Mashariki, imebeba abiria jumla ya 220,227 katika safari 576 wakati wa likizo ya siku 12 ya mwisho wa mwaka kuanzia Desemba 22 hadi Januari 2, Eva Chairunisa, Meneja Mkuu Katibu wa Biashara wa Kampuni ya PT Kereta Cepat Indonesia (KCIC), amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari huku akisema kuwa idadi hiyo ni asilimia 33 zaidi ya ile ya kuanzia mapema Desemba hadi mwanzo wa msimu wa likizo.
"Kwa ujumla, wastani wa idadi ya abiria kila siku wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ulifikia 19,000 hadi 20,000" Chairunisa amesema huku akiongeza kuwa idadi kubwa ya abiria ilirekodiwa Desemba 26 ikiwa na abiria 21,188, ikifuatiwa na Desemba 23 iliyokuwa na abiria 21,151.
Reli ya Mwendo kasi ya Jakarta-Bandung iliyojengwa na China, inayoitwa Whoosh na wenyeji, ilianza kutoa huduma ya kibiashara Oktoba 2023. Tangu wakati huo hadi Desemba 26, reli hiyo ilikuwa imefanya safari zaidi ya milioni 1.
Ikiwa na kasi ya kilomita 350 kwa saa, reli hiyo inaunganisha stesheni ya reli ya Halim iliyoko Jakarta na stesheni ya Tegalluar katika jiji la nne kwa ukubwa nchini Indonesia la Bandung, Jimbo la Java Magharibi.
Chairunisa amesema ongezeko la idadi ya abiria limetokana na mahitaji yanayoongezeka ya watu kutaka kujaribu Whoosh ili kufurahia likizo zao za mwisho wa mwaka.
Abiria wakiwa kwenye foleni ndani ya ukumbi wa kusubiria treni katika Stesheni ya Reli ya Halim mjini Jakarta, Indonesia, Oktoba 17, 2023. (Xinhua/Xu Qin)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma