

Lugha Nyingine
Sudan yamwita nyumbani balozi wake nchini Kenya kwa kupinga Kenya kupokea kiongozi wa RSF
KHARTOUM - Sudan imemwita nyumbani balozi wake nchini Kenya kupinga mapokezi rasmi ya Kenya kwa Kamanda wa Vikosi vya Mwitikio wa Haraka (RSF) Mohamed Hamdan Dagalo, shirika la habari la Sudan, SUNA limeripoti.
"Sudan imemrudisha balozi wake wa Nairobi kwa ajili ya mashauriano, kupinga mapokezi rasmi yaliyoandaliwa na serikali ya Kenya kwa kamanda wa wanamgambo waasi alipozuru Kenya juzi (Jumatano)," Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Al-Sadiq amenukuliwa. akisema katika habari hiyo.
"Kenya imesahau uhalifu wa kutisha uliofanywa na vikosi vya waasi, na uharibifu viliousababisha kwa miundombinu ya nchi, uwezo, na mali za raia," Al-Sadiq amesema.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Sudan pia ameishutumu Kenya kwa kuwaunga mkono na kuwakaribisha viongozi waasi na wafuasi wao, "pamoja na kula njama na mataifa yenye uadui wa kikanda dhidi ya Sudan."
Siku ya Jumatano, Rais wa Kenya William Ruto alimpokea Dagalo mjini Nairobi, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Dagalo nchini Uganda, Ethiopia na Djibouti.
Sudan imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya jeshi la nchi hiyo SAF na RSF tangu Aprili 15. Watu zaidi ya 12,000 wameuawa katika mapigano hayo, kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya mapema mwezi Desemba.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma