China yapinga taarifa ya pamoja kuhusu Mazungumzo ya Pande Tatu ya Eneo la Indo-Pasifiki ya Marekani, Japan na Jamhuri ya Korea

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 09, 2024

BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning siku ya Jumatatu kwenye mkutano na waandishi wa habari akijibu swali kuhusu taarifa ya pamoja iliyotolewa ya Mazungumzo ya pande tatu ya Eneo la Indo-Pasifiki kati ya Marekani, Japan na Jamhuri ya Korea (ROK), amesema, China inapinga vikali taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliyotolewa siku ya Jumatatu Januari 6 na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inaeleza kuwa nchi hizo tatu zinafuatilia madai ya China katika Bahari ya Kusini na "hatua yake ya zaidi", na kusema kuwa Marekani, Japan na ROK "zitaendelea kufanya ushirikiano wao wa usalama wa baharini na utekelezaji wa sheria kwa mujibu wa sheria ya kimataifa."

Nchi hizo tatu pia zimesisitiza kwamba amani na utulivu katika Mlango-Bahari wa Taiwan ni muhimu kwa usalama na ustawi katika jumuiya ya kimataifa.

Msemaji huyo amesema, "China imebaini mazungumzo ya Marekani na Japan na Jamhuri ya Korea na matokeo yake ya taarifa ya pamoja," na inafuatilia zaidi kauli zisizofaa zinazohusu China katika taarifa hiyo

"Tunapinga kwa uthabiti jaribio la nchi hizi la kuunda “kikundi kidogo” kwa jina la ushirikiano, kuingilia kimabavu mambo ya ndani ya China, kushambulia na kuipaka matope China na kuzusha mapambano na uadui," msemaji huyo amesema.

Amesema kuwa hivi sasa hali ya jumla ya Bahari ya Kusini ni shwari, na kwamba China inajikita katika kulinda mamlaka ya ardhi yake, na haki na maslahi yake ya baharini, huku ikishughulikia kwa mwafaka migongano kati yake na nchi zinazohusika moja kwa moja kwa kupitia mazungumzo na mashauriano.

"Nchi nyingine zisizo za kikanda zimejaribu kutanua misuli na kuchochea mapambano katika Bahari ya Kusini , hali ambayo haisaidii amani na utulivu katika kanda," amesema.

"Nataka kusisitiza kwamba Taiwan ni sehemu ya ardhi ya China isiyoweza kutengwa, suala la Taiwan ni mambo ya ndani ya China, na nchi yoyote hairuhusiwi kuingilia kati", Msemaji huyo amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha