

Lugha Nyingine
Mahakama ya Kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaidhinisha kuchaguliwa tena kwa Rais Tshisekedi
Picha ya kumbukumbu iliyopigwa Oktoba 3, 2023 ikimuonyesha Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi (katikati) akishiriki kwenye hafla iliyofanyika katika bandari ya nchi kavu ya Sakania ya Jimbo la Haut-Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. (Xinhua/Shi Yu)
KINSHASA - Mahakama ya Kikatiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Jumanne imethibitisha rasmi kuchaguliwa tena kwa Rais Felix Tshisekedi kuendelea kuwa rais wa nchi hiyo kufuatia uchaguzi wa Desemba 20 ambapo Tshisekedi alipata asilimia 73.47 ya kura zote halali zilizopigwa, huku mgombea mkuu wa upinzani Moise Katumbi akifuatia kwa kupata asilimia 18.08.
Rais huyo mteule amepangwa kuapishwa Januari 20 baada ya Mahakama ya Kikatiba kuidhinisha matokeo hayo ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC iliyosimamia uchaguzi huo mkuu, raia wa DRC zaidi ya milioni 18, kutoka wapiga kura jumla ya milioni 44 waliojiandikisha, walipiga kura katika uchaguzi wa rais, Bunge la Taifa na mabaraza 26 ya majimbo.
Hata hivyo, mchakato huo haukufanyika bila kuwa na utata kwani wagombea wa upinzani waliibua madai ya dosari, ambazo tume ya uchaguzi baadaye ilisema hazikuathiri matokeo ya uchaguzi.
Uchaguzi huo ulikuwa muhimu kwani ni wa pili kwa viongozi kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani katika historia ya nchi hiyo tangu ipate uhuru Mwaka 1960. Mwaka 2018, Tshisekedi aliingia madarakani baada ya kushinda uchaguzi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi kukabidhiana madaraka kwa amani nchini humo tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma